Wawekezaji wavutiwa sekta ya mifugo

13Aug 2019
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Wawekezaji wavutiwa sekta ya mifugo

MCHAKATO wa kuwaanda Watanzania kuzalisha kwa wingi malighafi ya viwandani wakati Tanzania ikielekea katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, umeanza kuwavutia wawekezaji wa sekta ya mifugo na mazao yake kuwekeza kulingana na mahitaji ya soko.

Kampuni ya Match Maker Tanzania ambayo inafanya kazi kwa karibu na Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV), linaloendesha mradi wa faida maziwa kwa wafugaji wa wilaya za Hai na Siha, mkoani Kilimanjaro, imeeleza nia yake ya kuendelea kuwawezesha wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kufuga kulingana na mahitaji ya masoko la maziwa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalumu, Mkurugenzi wa Kampuni ya Match Maker, Peniel Uliwa, ameeleza kuwa mpango wa huo una lenga kuchochea ajira, ustawi endelevu wa jamii na kufungua fursa za upatikanaji wa malighafi ya viwandani kupitia sekta ya mifugo na hasa ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa.

“Kimsingi tunaendelea kuwawezesha wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kufuga kulingana na mahitaji ya masoko la maziwa ndani na nje ya nchi kwa kuwahimiza vijana kujiunga katika vikundi ili iwe rahisi kupata fursa za mikopo zitakazowasaidia kupanua wigo wa miradi yao ya kiuchumi.

“Yako mambo mengi sana yanaweza kusimamiwa na wadau wengine wanaoweza kuisaidia Serikali ya Tanzania kufikia ndoto zake, mfano ni kuboresha mazingira na usimamizi wa uwekezaji wa sekta binafsi hasusani viwanda vya kusindika maziwa, nyama, ngozi, samaki, mafuta ya kula, madawa na vifaa tiba, vyakula vya binadamu na mifugo.”

Alisema moja ya mambo ambayo hivi sasa wanayakazia wanapokutana na wananchi na hasa wafugaji ni ubora wa uhifadhi wa malisho mabichi ya mahindi kwa ajili ya chakula cha mifugo maarufu kama sailage.

Ubora katika uhifadhi wa malisho hayo, husaidia kuruhusu kuhifadhi karibu viinilishe vyote vilivyo kwenye mimea ambavyo vinatajwa kuongeza tija ya maziwa kwa asilimia 15.

Wakati wadau hao wakihimiza pia matumizi ya teknolojia kwenye tasnia ya maziwa, baadhi ya wataalam wa mifugo akiwamo Marijan Kizigha wametaka kuwapo na njia mbadala ya kufikia ndoto hizo kwa serikali kuainisha sera na mikakati ya kuongeza mapato.

Alizitaja njia hizo kuwa ni kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato vilivyopo hususani katika matumizi ya mifumo ya kielektroniki, kuongeza wigo wa kodi kwa kurasimisha sekta isiyo rasmi, kuboresha mazingira ya uwekezaji na urasimishaji ili kuvutia biashara na uwekezaji ukiwamo.

Nyingine ni kuboresha miundombinu, vivutio vya kodi, sera thabiti zisizobadilika mara kwa mara, upatikanaji wa ardhi na uwapo wa taratibu za kisheria na usimamizi bora pamoja na kuimarisha ushirikiano na washirika wa maendeleo.