Kilimanjaro yatajwa kinara matukio ukatili

13Aug 2019
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Kilimanjaro yatajwa kinara matukio ukatili

MKOA wa Kilimanjaro unatajwa kuwa miongoni mwa mikoa 10 nchini ambayo ni kinara wa matukio ya ukatili na unyanyasaji wa wanawake na watoto wa kike.

Kwa mujibu wa Ofisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Moshi, Magreth Reuben, kundi la watoto wa kiume pia liko katika hatari ya kuathiriwa na vitendo hivyo kutokana na viashiria na idadi ya matendo ya kinyama yanayojitokeza hivi sasa.

Hayo yamo katika taarifa yake aliyoitoa, wakati akizungumza na wanaharakati wanaounda jukwaa la mashirika yasio ya kiserikali mkoani Kilimanjaro.

Alisema matukio makubwa kwa sasa ni ubakaji, ulawiti na ngono zembe kwa watoto wenye umri mdogo.

Pia, aliyataka mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotoa huduma katika jamii kwa asilimia 80 kutenga bajeti za kuhakikisha yanawafikia jamii kwa karibu na kutoa elimu za kufichua vitendo viovu vinavyofanyiwa watoto pamoja na wanawake  sehemu wanazoishi.

 Katika mkutano na jukwaa hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi, alisema halmashauri hiyo kwa sasa ndiyo inaonekana kuwa kinara wa matukio ya ukatili.

Kutokana na kasi ya matukio ya ukatili, Mwandezi ameyataka mashirika hayo kutoa elimu kwa jamii na kufuatilia kwa karibu kesi za unyanyasaji na ukatili wa kijinsia ambazo zinawagusa wanawake na watoto.

Nao baadhi ya wanaharakati Mkoa wa Kilimanjaro wakitoa maoni yao katika jukwa hilo, walikiri kuwapo kwa matukio ya ukatili na kwamba changamoto kubwa wanazokutana nazo katika kukabiliana na matukio hayo ni pamoja na kesi nyingi zinazopelekwa mahakamani kumalizika kiaina, baada ya ndugu na jamaa kurudisha kesi hizo nyumbani.

Habari Kubwa