Waturuki waitwa kuwekeza Singida

14Aug 2019
Jumbe Ismaily
SINGIDA
Nipashe
Waturuki waitwa kuwekeza Singida

SERIKALI imetoa wito kwa wawekezaji kutoka Uturuki kuwekeza kwenye sekta ya kilimo na ufugaji wilayani Singida ili kuwezesha upatikanaji wa ng’ombe na mbuzi wengi kutoka kwenye mashamba yaliyopo.

Akizindua kwa niaba yaa Mkuu wa Wilaya ya Singida, Pascas Muragiri katika ugawaji kitoweo cha wanyama waliochinjwa kwa ajili ya kutolewa sadaka kusherehekea sikukuu ya Eid-Elhaji, Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida, Wilson Shimo, alisisitiza kwamba ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Uturuki haukuanza leo, bali ulianza  tangu uongozi wa  Baba wa Taifa, Hayati  Mwalimu JuliusNyerere.

Shimo alitumia uzinduzi huo kuwakaribisha wawekezaji hao kuja kuwekeza katika fursa zingine za kiuchumi na kiuwekezaji katika Wilaya ya Singida.

Akitoa taarifa fupi ya shughuli ya chinjo iliyofanyika katika Msikiti wa Alshababu, Mtaa wa Unyakindi, Manispaa ya Singida, Mudiri wa Jimbo la Singida, Zuberi Saidi Mkoko, alifafanua kwamba katika siku ya kwanza ya zoezi hilo walichinja jumla ya wanyama 1,410 wakiwamo ng’ombe 160 na mbuzi 1,250 wakati kwenye msikiti wa Mtaa wa Misuna uliopo kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani walichinja wanyama 1,310 wakiwamo ng’ombe 60 na mbuzi 1,250.

Amiri wa Jumuiya ya Answari Suna Tanzania (JASUTA ) Mkoa wa Singida, Yahaya Mohamed, alisema shughuli za uchinjaji na ugawaji wa kitoweo hicho wamekuwa wakiifanya kwa kuzingatia zaidi ubinadamu, na siyo masuala ya itikadi na kwamba watu watakaopata bahati ya kitoweo ni watu wa aina zote,  wa dini zote, wa rangi zote na wa makabila yote.