DC awasifu viongozi kuhamasisha maendeleo

14Aug 2019
Jaliwason Jasson
MANYARA
Nipashe
DC awasifu viongozi kuhamasisha maendeleo

MKUU wa wilaya ya Babati, Elizabeth Kitundu, amewashukuru   viongozi wa dini  kwa kusaidia  serikali kuhamasisha maendeleo kwa haraka kwenye jamii wanazoziongoza.

MKUU wa wilaya ya Babati, Elizabeth Kitundu

Hayo alisema  jana Kitundu  katika Baraza la Idd, lililofanyika mjini Babati katika uwanja wa Kwaraa.

"Hakika bila ninyi viongozi wa dini kufanya kazi nzuri ya kuwaambia  wananchi kuhusu maendeleo , kazi yetu sisi viongozi wa serikali ingekuwa ngumu sana maana tusingeweza  kufanikisha wala kutawala kwa amani,"alisema Kitundu

Aidha, aliwataka viongozi wa Kiislamu kuendelea kuwahimiza vijana kuepuka kufanya vitendo viovu  kama vile wizi na kucheza kamari, bali wafanye kazi zilizo halali kwa kufuata sheria na kutumia vitambulisho vya wajasiriamali.

Mkuu wa wilaya  aliwaomba kuendelea kuwahamasisha wananchi kumuunga mkono Rais John Magufuli, katika jitihada zake za kuiletea nchi maendeleo na  pia kuhimiza waumini wao kushiriki uchaguzi  wa serikali za mitaa  na vijiji.

"Kwani Rais wetu anastahili kuungwa mkono kwa sababu ni mchapakazi na hivyo tumchague na kumpa wasaidizi wake uchaguzi wa mwaka huu wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani,"alisema

 Shekhe wa Mkoa wa Manyara, Mohamed Kadidi, aliwataka  waislamu kujitathimini wamefanya nini kwa mwaka mzima na wajikite kwenye mipango ya maendeleo na si vinginevyo.

Shekhe Kadidi aliwaambia kuwa misikitini siyo ni sehemu ya kufanya migogoro au fitina, bali wanatakiwa kupendana na kuchapa kazi kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao na taifa pia.

Katibu wa Baraza la Waislamu (Bakwata) Wilaya ya Babati , Abdi Issuja,  akisoma risala alisema miongoni mwa changamoto inayowakabili ni ukosefu wa usafiri na kuwaomba wadau kuchangia, ili waweze kuwafikia waumini kiurahisi.

Baada ya risala hiyo viongozi wa serikali na wa dini walichangia fedha taslimu  Shilingi  460,000 na ahadi zaidi ya Shilingi 2,000,000 kwa ajili ya kumaliza deni la  5,000,000   la gari waliyonunua  kwa ajili ya kufanya huduma kwa waumini wao.

Habari Kubwa