Wafugaji wahimizwa kusomesha watoto

14Aug 2019
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Wafugaji wahimizwa kusomesha watoto

WAFUGAJI katika mikoa mbalimbali wameshauriwa kuwekeza zaidi katika elimu kwa watoto wao  bila kujali jinsia kwani wote wana haki sawa ya kuondokana na ujinga.

Aidha, wamekumbushwa kuachana na mfumo  dume wa kuwapeleka watoto wa kike machungani na kuwapendelea zaidi watoto wa kiume.

Hayo yalisemwa jana na mdau wa elimu ,Paulo Ndari, wakati akizungumza katika sherehe za kimila za kumsimika  kiongozi wa boma katika Kijiji cha Engaroji Kata ya Lepuko Wilayani Monduli mkoani Arusha.

Alisema kuwa,jamii nyingi za wafugaji wamekuwa wakiendekeza mfumo dume, kwa kuwabagua watoto katika utoaji wa elimu, ambapo wamekuwa wakiwapendelea watoto  wa kiume, huku watoto wa kike wakiishia kuchunga na kubaki majumbani.

Alisema  umefika wakati sasa wa jamii hiyo kuachana na mifumo dume,  badala yake wawekeze katika elimu kwa watoto wote bila ubaguzi, kwani zawadi pekee wanayotakiwa kupewa watoto hao ni elimu na sio vinginevyo.

"Sisi  viongozi katika jamii yetu tuna majukumu makubwa sana ya kuhakikisha watoto  wote wanapata haki sawa, huku tukiweka sheria zetu za kuwabana wale wote wanaokiuka sheria hizo, ikiwemo suala zima la elimu na tumepiga marufuku kwa mtoto yoyote kwenda machungani, hivyo  watoto wote lazima waende shuleni  na akitokea mtu yeyote amekiuka anapigwa faini,"alisema Paulo.

Alifafanua kuwa, bado kuna changamoto kubwa ya elimu katika jamii hiyo ya kifugaji kutokana na wengi wao  kutojua umuhimu  wa kuwekeza katika elimu, ambapo wamekuwa wakiendelea kuelimisha jamii yao kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa kimila .

Kwa upande wake kiongozi wa kimila Laigwanani wa kijiji hicho, Bukula Narida, alisema kuwa,wamekuwa wakichagua viongozi hao katika jamii zao, kwani wana wajibu  mkubwa na mchango katika kuleta mabadiliko ndani ya jamii.

Aidha, alisema kwa kutumia sheria zao ndogo ndogo walizojiwekea viongozi hao wanahusika kudhibiti mila zisizo rafiki na kuhimiza masuala ya serikali yanayosimamia maendeleo ya jamii.

Narida aliongeza kuwa,kupitia viongozi hao jamii hiyo ya wafugaji imeweza kuelimika na kupeleka watoto shuleni, japo  bado kuna changamoto  katika kuwepo kwa haki sawa kwa watoto wote bila kuwepo kwa ubaguzi wowote.

"Tumejiwekea  sheria ndogondogo za kuwabana wote wanaokwenda  tofauti na makubaliano yetu na zimekuwa zikisaidia sana, kwani yoyote anayeenda kinyume huwa anapigwa faini, kulingana na sheria zetu na wengi wao wamekuwa wakijirekebisha sana,"alisema.

Mwananchi mwingine, Sanare Mollel, alisema kuwa, uwepo wa viongozi hao katika jamii unasaidia  kushawishi watu katika suala zima la maendeleo, pamoja na  kutatua migogoro mbalimbali inayotokea ndani ya jamii kabla ya kwenda kwenye ngazi za juu, kwani viongozi kama hao ndio wanaaminika zaidi tofauti na wengine hasa katika jamii za kifugaji.

Kiongozi mwingine wa kimila Laigwanani, Loshiro Mollel, alizitaka jamii  mbalimbali kuendelea kuzienzi na kuzithamini mila na desturi zao, kuhakikisha zinadumishwa ili ziendelee kutumiwa na vizazi vijavyo kwa lengo la kujiletea maendeleo katika jamii yao.