Wananchi waiomba serikali umeme

14Aug 2019
Cynthia Mwilolezi
MANYARA
Nipashe
Wananchi waiomba serikali umeme

WAKAZI  wa Kata ya Terrat wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara, wameiomba serikali kufikisha umeme kwani viwanda na miradi ya maendeleo inakwama.

Waliomba kupitia awamu ya tatu ya mpango wa usambazaji wa nishati ya umeme vijijini wapate nishati hiyo, ili visima na viwanda vidogo viweze kukamilika na kuwanufaisha kiuchumi.

Wananchi hao waliyasema hayo juzi wakati wakizungumza kwenye kijiji cha Terrat wakati wa kikao cha kuzungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa na kumpongeza Rais John Magufuli kwa kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya kimkakati.

Katika kikao hicho kilichohusisha viongozi wa CCM wa Kata  za Komolo, Terrat na Oljoro namba tano za Tarafa ya Terrat, walisema umeme ukiwafikia watanufaika zaidi tofauti na sasa wanapotumia nishati ya umeme wa juaa -sola na jenereta.

Diwani wa Kata ya Terrat, Jackson Ole Materi, alisema katika mpango wa visima 20 vya wilaya hiyo, kata hiyo ilifanikiwa kupata visima viwili ila wanashindwa kuviendesha kutokana na ukosefu wa nishati ya umeme.

"Rais John Magufuli kupitia ilani ya CCM anatekeleza jukumu la  kumtua mwanamke ndoo kichwani lakini tunashidwa kutekeleza hilo kwa ukosefu wa umeme, ila tuna matarajio utafika na maji yatakuwepo kwa wingi," alisema Ole Materi.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa wa Wilaya ya Simanjiro Daniel Ole Materi alisema, kiwanda cha maziwa kimeshidwa kufanya kazi kutokana na kutowepo kwa nishati ya umeme.

"Gharama za umeme wa jua na jenereta ni ghali mno katika kuendesha viwanda, tunaiomba serikali ifanikishe hili suala la umeme wa vijijini Rea kwani ni hitaji kubwa kwa jamii," alisema Ole Materi.

Ofisa Tarafa ya Terrat, Lekshon Kiruswa alisema suala la mradi wa Rea awamu ya tatu kwenye eneo hilo unaendelea vizuri, kwani vijiji vingi katika tarafa hiyo vimepata umeme.

Kiruswa alisema  kata za Oljoro namba tano na Komolo zimeshapata nishati  ya umeme na hivi sasa unaelekea Kijiji cha Nadonjukin, kisha utaingia Kata ya Terrat na kuendelea kusambazwa katika vijiji vya eneo hilo.

Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha hadi ifikapo mwaka 2021 vijiji vyote nchini viwe vimefikiwa na nishati ya umeme  wa Rea na kutokana na kasi kubwa inavyokwenda utekelezaji wake utafanikiwa.

Mkazi wa Kijiji cha Terrat Jacob Laizer alisema endapo umeme ungefika katika eneo hilo hivi sasa kungekuwa na maendeleo makubwa mno.

"Kuna wafugaji wana uwezo wa kufungua viwanda vidogo ili kumuunga mkono Rais John Magufuli katika dhana ya Tanzania ya viwanda, ila wanashindwa kutokana na ukosefu wa nishati ya umeme," alisema Laizer.

Habari Kubwa