Wataka utafiti wa kina Ziwa Chala

14Aug 2019
Godfrey Mushi
ROMBO
Nipashe
Wataka utafiti wa kina Ziwa Chala

BAADHI ya wadau wa sekta ya utalii mkoani Kilimanjaro, wameishauri Wizara ya Maliasili na Utalii, itenge fungu maalum kwa ajili ya kufanya utafiti wa kisayansi utakaothibitisha kina halisi cha Ziwa Chala ambalo linatembelewa na idadi kubwa ya wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Ziwa Chala

Ziwa hilo liko mpakani mwa nchi ya Kenya na Tanzania, takribani kilomita 45 kutoka barabara kuu ya Moshi-Taveta.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana baada ya kufanya utalii wa ndani, wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Eid el Hajj, akiwamo mwongoza watalii Vallerian Mboya, walisema licha ya ziwa hilo kudaiwa kuwa na muunganiko wa kijiolojia na Mlima Kilimanjaro, iko haja kwa serikali kuwa na kanzi data inayoonyesha kina halisi cha ziwa hilo ili kutoa fursa ya watalii kupata taarifa sahihi.

"Ukiangalia karibu asilimia 60 ya watalii wanaotembelea Ziwa Chala kwa upande wa wilaya ya Rombo wanatuuliza maswali kuhusu kina cha ziwa hili lakini hatuna majibu. Tunaishia kuwaeleza kwamba bado hakujafanyika utafiti kujua ukubwa wake kwenda chini," alisema Mboya.

Hata hivyo, inaelezwa kwamba ziwa hilo lina takribani kina cha mita 3,000 lakini hakuna utafiti wa kisayansi unaothibitisha urefu wa ziwa hilo ambalo lina mvuto wa kipekee kwa kuwa hakuna mto unaoingiza wala kutoa maji. Ni ziwa lenye maji baridi na samaki wa maji baridi.

Naye Isaack Nuru maarufu kama Zedane, ambaye ni mwongoza watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, akiwa katika ziwa hilo, alisema pamoja na kwamba uko mwamko mkubwa wa wananchi kutembelea vivutio vya utalii, ni vyema serikali ikafanya utafiti huo kujiridhisha.

Katika tovuti ya Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, taarifa iliyowekwa inaeleza kuwa eneo la Ziwa Chala kuna hekta zipatazo 23 kwa upande wa Tanzania ambazo ni mashamba yanayomilikiwa na watu binafsi ambako kunaweza kutumika kwa ujenzi wa hoteli na ‘campsite’.

Moja ya maajabu ya Ziwa Chala ambalo ndilo kivutio kikuu cha utalii katika Wilaya ya Rombo, ni uwezo wake wa kutopungua maji, wala kuongezeka kipindi cha mvua au ukame, huku kukiwa hakuna mto unaoingiza maji katika ziwa hilo.

Ziwa hilo lililoko katika Kijiji Malowa, lina ukubwa wa hekta 421, huku utafiti mbalimbali wa kitaalamu ukieleza chanzo chake ni kimetokana na mlipuko wa volkano uliosababisha ardhi kudidimia na hatimaye kuwa na bonde kubwa la maji yakitokea chini kwa chini kwenye miamba.

Habari Kubwa