Hai yatenga eneo la uwekezaji

14Aug 2019
Godfrey Mushi
HAI
Nipashe
Hai yatenga eneo la uwekezaji

SERIKALI wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro imetenga eneo la ukanda maalum wa viwanda (EPZ) lenye ukubwa wa hekta 463 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vikubwa.

Taarifa iliyothibitishwa na Halmashauri ya Wilaya ya Hai na kuwekwa katika tovuti ya serikali, inaeleza kuwa eneo hilo liko katika barabara kuu ya Moshi- Kilimanjaro.

Kutokana na taarifa hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya, alipoulizwa na Nipashe ni eneo gani ambalo ni mahususi kwa ajili ya uwekezaji huo, alisema katika eneo la Mashine Tools, njia panda ya Machame. Eneo hilo limetengwa hekta 430 kati ya 463.

Kwa mujibu wa Ole Sabaya, eneo hilo hivi sasa limewekwa wazi kwa ajili ya uwekezaji wa bidhaa za viwandani.

Kuhusu uwekezaji katika sekta ya utalii, alisema wilaya hiyo ina vivutio muhimu  ambavyo ni pamoja na chemuchem ya Chekimaji inayotoa maji ya moto.

"Hai yako pia maeneo ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji wa hoteli za kitalii hasa ukizingatia ni eneo lililo karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Hivi sasa tunahangaika kutafuta wawekezaji ndani na nje ya nchi ambao watakuja kuwekeza hapa kwa ajili ya kuchochea sekta ya utalii," alisema.

Kuhusu mchakato wa utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimkakati wa ujenzi wa soko la kimataifa la nafaka ambalo uwekezaji wake utagharimu Sh. bilioni 11 katika eneo la Kwa Sadala, Ole Sabaya alisema unaendelea kwa kasi na wakati wowote atatangaza kuanza kwa ujenzi wake.

Soko hilo ambalo limepewa jina la 'The Magufuli International Complex Centre' (MICC-Hai), litajengwa karibu na kiwanda cha Arsho au mkabala na njia panda ya kwenda Masama.

Inaelezwa kuwa soko hilo ambalo litakuwa na kazi ya kuongeza thamani ya mazao, kuchochea pato la mkulima na kuingizia serikali kodi, litakuwa na eneo maalum la viwanda vya usindikaji, eneo la utalii zikiwamo hoteli, kituo cha habari za utalii, migahawa ya kisasa na maeneo ya huduma za kibenki.

Pia litakuwa na ofisi za bima, kumbi za kisasa za mikutano na maduka makubwa. Muda ambao mradi huo utatekelezwa ni miaka miwili na utagawanyika katika awamu tatu.

Habari Kubwa