Kakolanya ashusha presha ya Aussems kwa Manula

14Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kakolanya ashusha presha ya Aussems kwa Manula

UWEZO unaoonyeshwa na kipa mpya wa Simba, Beno Kakolanya, umezidi kumshawishi Kocha Mkuu wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara, Mbelgiji Patrick Aussems, jambo ambalo limemfanya kueleza anaona changamoto kubwa kwa mlinda mlango namba moja, Aishi Manula.

kipa mpya wa Simba, Beno Kakolanya

Manula ambaye hajaichezea Simba tangu aiache kambini Afrika Kusini na kurejea kujiunga na Taifa Stars, kukosekana kwake kumetoa nafasi kwa Kakolanya kuweza kuonyesha ubora wake ambao sasa umemshawishi Aussems.

Mbali na mechi za kirafiki Kakolanya alizosimama langoni wakiwa kambini Afrika Kusini na kufanya vizuri, ameidakia Simba pia katika mechi ya kirafiki dhidi ya Power Dynamos ya Zambia iliyopigwa Uwanja wa Taifa kwenye kilele cha Simba Day na kumalizika kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara kushinda 3-1.

Katika mechi ya kimashindano ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya UD Songo iliyomalizika kwa sare tasa ugenini Beira nchini Msumbiji, pia Kakolanya ndiye aliyesimama langoni na kuonyesha uwezo mkubwa kwa kufuta makosa kadhaa yaliyofanywa na safu ya ulinzi.

Kutokana na kiwango hicho, Aussems amemsifu Kakolanya kwa kufanya vizuri, na kueleza kuwa kwa sasa hana wasiwasi tena kama ilivyokuwa msimu uliopita wakati Manula alipoumia.

“Katika mechi zote alizocheza,  amefanya vizuri, hivyo ni matumaini yangu kadiri siku zinavyoenda atakuwa bora zaidi na natarajia atatoa changamoto kubwa kwa Manula," alisema Aussems alipoulizwa kuhusu kiwango cha Kakolanya.

Habari Kubwa