Matola kuiongezea kasi Yanga Ijumaa

14Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Matola kuiongezea kasi Yanga Ijumaa

BAADA ya kuipa tabu Yanga wakati akiinoa Lipuli FC ya Iringa, Kocha wa Polisi Tanzania, Seleman Matola, Ijumaa atakipima ubavu kikosi chake hicho kwa kucheza na vijana hao wa Mwinyi Zahera katika mechi ya kirafiki itakayopigwa Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Yanga

Yanga jana imeelekea mkoani Kilimanjaro kuweka kambi ya kujiandaa na mechi yao ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers itakayopigwa Agosti 24, mwaka huu mjini Gaborone, Botswana.

Uongozi wa Yanga juzi, ulieleza kuwa umeamua kuweka kambi Kilimanjaro ili kuweza kuzoea hali ya baridi ambayo inaelezwa kufanana na ile ya Botswana kwa sasa, na ikiwa huko itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania ili kutafuta kasi ya kukivaa Township Rollers ambayo walipelekana mchakamchaka kwenye mechi ya awali Uwanja wa Taifa na kutoka sare ya bao 1-1.

Aidha, Polisi Tanzania nayo imesema itautumia mchezo huo utakaopigwa majira saa 10 alasiri kwa kutambulisha wachezaji wake wa msimu huu, kutambulisha jezi na benchi zima la ufundi.

Msimu uliopita wakati akiinoa Lipuli, Matola alikubali kipigo cha bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu raundi ya kwanza iliyopigwa Uwanja wa Taifa kabla ya kuigeuzia kibao raundi ya pili kwa kupata ushindi kama huo kwenye dimba la Kumbukumbu ya Sokoine mjini Iringa.

Kisha Matola aliiwezesha Lipuli kuitupa Yanga nje kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho nchini (FA Cup) kwa kuichapa mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wao wa Kumbukumbu ya Sokoine.

Akizungumzia maendeleo ya kikosi chake kilichokuwa kimeweka kambi jijini Dar es Salaam kujiandaa na Ligi Kuu inayotarajiwa kuanza Agosti 23, Matola alisema wamefanya maandalizi mazuri na ana imani kubwa ya kutoa upinzani kwa timu zote ikiwamo kwa vigogo wa soka nchini Simba, Yanga na Azam FC.

“Tumejiandaa vizuri, wachezaji wana ari ya kutosha kabla ya ligi kuanza, hivyo tunaamini tutafanya makubwa msimu utakapoanza hasa ukizingatia ni kikosi kipya, lazima wachezaji wawe na mambo mapya.

“Kwa ujumla hatuna hofu hata dhidi ya Simba, Yanga, Azam tunaweza kupambana na kupata matokeo," alisema.

Habari Kubwa