Vifo ajali mafuta sasa vyafikia 76

14Aug 2019
Christina Haule
MOROGORO
Nipashe
Vifo ajali mafuta sasa vyafikia 76

VIFO vya watu wa ajali ya moto vilivyosababishwa na lori la mafuta lililopinduka eneo la Msamvu mkoani Morogoro vimefikia 76, baada ya majeruhi mmoja wa Hospitali ya Muhimbili kufariki dunia juzi usiku.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe, miili minane ipo chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Rufani mkoani Morogoro.

Alisema kati ya miili minane iliyopo chumba cha kuhifadhia maiti, sita imeshatambuliwa.

Dk. Kebwe alisema, juhudi za kupima vinasaba (DNA) kwa utambuzi wa wagonjwa na miili iliyobakia zinaendelea na kwamba jumla ya wagonjwa 38 wapo Hospitali ya Rufani Muhimbili wakiendelea na matibabu, huku 16 wakiwa Hospitali  ya Rufani Morogoro.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenister Mhagama, alisema  bado wanaendelea na suala la utambuzi, mazishi, tiba na tiba ya kisaikolojia.

Alisema, tayari wameshapokea wataalamu wa saikolojia kwa ajili ya kutoa tiba hiyo. Vile vile, alisema timu ya maafa ya taifa imekabidhi rasmi kwa kamati ya maafa ya mkoa kuendelea na shughuli zilizobakia huku ikisimamia utekelezaji.

Alisema, shughuli mbalimbali bado zinaendelea ikiwamo mazishi kwa miili inayotambuliwa na serikali na hata wanaozikwa na ndugu zao.

Pia alisema  kamati ya maafa itachukua muda mrefu kwa sababu wagonjwa bado wanaendelea kutibiwa huku wakihitaji uangalizi.

Akizungumzia tume ya wiki moja ya kuchunguza hali ya ajali iliyoundwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliwataka wananchi kuwa watulivu na kusubiri matokeo ya tume hiyo ambayo mpaka sasa ipo kazini.

Mmoja wa wataalamu wa saikolojia, Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Dk. Naftali Ng'ondi, alisema wamekuja kutoa msaada wa kisaikolojia kwa kuanzia na kufanya utambuzi wa familia zilizopoteza ndugu zao na kuangalia mahitaji kwa familia hizo, majeruhi na ndugu zao.

Dk.  Ng'ondi alisema, mpaka sasa wameshapata taarifa ya vifo vya watu 76 na wagonjwa 56 waliopo hospitalini.

Alisema wameamua kutoa msaada wa kisaikolojia kwa wafiwa na wagonjwa kufuatia tukio likilotokea kuwa la kushtukiza ambalo linauwezekano mkubwa wa kuleta msongo wa mawazo na hivyo kurudishwa kwenye hali ya kawaida.

Misaada mbalimbali imeendelea kutolewa ikiwamo Benki ya CRDB Mkoa wa Morogoro na Ofisi ya Maji, Bonde la Wami Ruvu.

Watu, taasisi na makundi mbalimbali yameendelea kutoa damu katika Kituo cha Damu Salama na msimamizi wa kituo hicho, Angel Sengati, alisema mpaka sasa wamekusanya chupa 382 na wanaendelea kupokea makundi mengine ya watoa damu.

Habari Kubwa