Mamia wajitokeza upasuaji kupunguza ukubwa matiti

14Aug 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mamia wajitokeza upasuaji kupunguza ukubwa matiti

MADAKTARI bingwa kutoka Hospitali ya Aga Khan na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na wenzao wa Marekani, Canada na nchi za Ulaya, wamefanya upasuaji wa kwanza Tanzania wa kupunguza ukubwa wa matiti.

Imeelezwa kuwa tayari wanawake 150 wamejitoleza kupatiwa matibabu hayo ya kibingwa huku yakifanyika kwa mafanikio makubwa kwa mmoja wao.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya Aga Khan, Aidan Njau, alitangaza neema hiyo jijini Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari wakati kambi ya madaktari hao ikiwa Aga Khan kwa ajili ya upasuaji huo.

Alisema timu ya wataalamu hao ilianza kambi yake Jumapili ikifanya upasuaji huo wa matiti makubwa na kurekebisha makovu yaliyotokana na ajali mbalimbali yakiwamo ya moto.

Dk. Njau alisema mpaka jana, walikuwa wamefanikiwa kufanya upasuaji huo kwa mwanamke aliyekuwa na matiti makubwa na kuyaweka matiti yake kwa kiwango alichotaka.

"Leo (jana) tumefanya upasuaji mkubwa, tangu saa moja asubuhi hadi wakati huo (saa sita mchana) tulikuwa tunamfanyia upasuaji mwanamke mwenye matiti makubwa kwa kiwango alichokitaka kwa sababu yanamtesa na kumuumiza mgongo na kukosa mwonekano mzuri," alisema.

Alisema mwitikio wa wanawake wanaotaka kufanyiwa upasuaji huo ni mkubwa, akibainisha kuwa wakati wanafanya uchunguzi, walijitokeza karibu wagonjwa 150.

"Kwa sasa tumemfanyia mwanamke mmoja, awamu nyingine inayotarajiwa kufanyika Novemba, tunatarajia kuwafanyia wanawake wengine wanne. Upasuaji huu siyo kazi ndogo kwa sababu unalenga kumremba mtu kwa mwonekano anaoutaka mhusika na unahitaji umakini wa hali ya juu ili kumridhisha mgonjwa kwa kile anachokihitaji," alisema.

Alisema hospitali hiyo kwa miaka mitano iliyopita imekuwa ikifanya upasuaji kwa wanawake wenye saratani ya matiti na baadaye kuwatengenezea mengine ya bandia.

"Tunafanya hivi ili akirudi kwenye jamii yake aendelee kuonekana kwa mwonekano wake wa awali badala ya kutengwa kwa kuwa na mwonekano tofauti, mwitikio ni mkubwa, tulikwenda hadi mikoani kuwaangalia wagonjwa, wengi wana matatizo," alisema.

Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Marekani, Andrea Pusic, ambaye ni mkuu wa shirika la kimataifa lisilo la kiserikali la kusaidia wanawake, alisema changamoto walizokutana nazo ni pamoja na wingi wa wahitaji wa huduma hiyo na wamelazimika kuchukua wenye uhitaji mkubwa zaidi.

Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano, Olayce Lotha, alisema gharama iliyotumika katika awamu hiyo ya tano ya matibabu hayo ni Sh. milioni 285.6 ambazo zimepatikana kupitia wadau mbalimbali na wanufaika 56 wanaofanyiwa upasuaji wa makovu ya moto.

Mwanzilishi wa Mtandao wa Sadaka, Dk. Ibrahim Msengi, alisema wanashirikiana na serikali na taasisi mbalimbali kusaidia wagonjwa wanaohitaji kutibiwa makovu yanayotokana na ajali.

Habari Kubwa