Kabudi aahidi kukipaisha Kiswahili SADC

14Aug 2019
Beatrice Moses
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kabudi aahidi kukipaisha Kiswahili SADC

MWENYEKITI mpya wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Profesa Palamagamba Kabudi, amesema nchi wanachama zinahitaji kuelekeza nguvu katika kufanikisha mapinduzi ya viwanda ili kuzalisha ajira nyingi.

MWENYEKITI mpya wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Profesa Palamagamba Kabudi

Profesa Kabudi ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema nguvu hizo pia zinahitajika kwenye uzalishaji mali na uboreshaji wa miundombinu, hatua ambayo itasaidia vijana wengi kupata ajira.  

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akihutubia baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa Kamati ya Baraza hilo, nafasi ambayo atadumu nayo kwa kipindi cha mwaka mmoja. 

Profesa Kapudi alisema ni wazi kwamba umoja unahitajika ili kufanikisha azima hiyo, kwa kuwa hakuna nchi inayoweza kujitegemea na kupata mafanikio kwa wakati badala yake itakuwa inajichelewesha.

"Ushirikiano huu utasaidia katika kuweka na kusimamia sera wezeshi kwenye uwekezaji na ujenzi wa viwanda nchi za SADC," Profesa Kabudi, alisema.

Kadhalika, alisema katika kutekeleza hilo, juhudi za dhati zinahitajika ikiwamo kuwa na sera wezeshi pamoja na kushughulikia na kuondoa vikwazo vya kibiashara katika maeneo yote ya nchi wanachama.

Akizungumzia wadhifa aliopewa, Profesa Kabudi alisema anaona fahari kupokea kijiti hicho cha uongozi kwa kuwa nafasi ya Tanzania katika SADC ni ya kipekee na ya kihistoria katika nchi hizo.

Alisema anapokea jukumu hilo kwa moyo mkunjufu, tena kwa heshima kubwa.

"Zaidi tunaishukuru Jamhuri ya Watu wa Namibia kwa kusimamia vyema nafasi hii kwa mwaka mzima uliopita," alisema Profesa Kabudi.

Profesa Kabudi anapokea nafasi hiyo kutoka kwa Naibu Waziri Mkuu wa Namibia anayeshughulikia Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa, Netumbo Ndaitwah, aliyekuwa mwenyekiti baraza hilo mkutano wa 38 wa SADC, ambayo inamaliza muda wake rasmi wiki hii.

Alisema kwa kukabidhiwa nafasi hiyo anakumbuka jukumu zito la Tanzania katika mkutano huo wa 39 wa SADC ambalo Tanzania ililibeba katika ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika na kulifanikisha.

Alisema Tanzania ilitumika katika kuwahifadhi na kuwapa mafunzo wanaharakati wa ukombozi. Kambi zao zilikuwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo Mazimbu, Kongwa, Nachingwea na Mgagao.

"Wakati huu tunapofanya mkutano huu wa 39 tunakumbuka pia miaka 20 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere, kama kiongozi wa harakati za ukombozi na alichangia katika kuanzishwa kwa umoja huu," Profesa Kabudi alisema.

Aliahidi kuhakikisha anaongoza katika kusongesha mbele mambo manne, ikiwamo kampeni ya kufanikisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya SADC, wakizingatia historia kwamba ni lugha iliyotumika kwa ukombozi.

"Hatuna sababu ya kusema tunaleta Kiswahili kama jambo jipya. Tunalofanya sasa ni kwamba hii ni lugha ya ukombozi waliyoitumia wakati wa kupigania uhuru, sasa iwe moja ya lugha rasmi SADC," alisema.

Alisema kuna mwitikio kwa lugha ya Kiswahili kwa kuwa tayari imeanza kutumika katika kufundishwa kwenye zaidi ya vyuo 58 duniani, pia ni miongoni mwa lugha kumi zinazozungumzwa duniani na watu wengi.

"Hivyo Tanzania itatilia mkazo isiwe lugha ya Afrika Mashariki pekee, bali iwe ya SADC na hatimaye lugha unganishi na jumuishi ya bara lote," alisema.

Profesa Kabudi alisema pia wapo kwenye harakati za kutaka jumuiya ya kimataifa kuondoa vikwazo vya kiuchumi kwa Zimbabwe.

"Uongozi uliopo Zimbabwe umechaguliwa kwa demokrasia, hivyo kuna haja ya kuiondolea vikwazo vya kiuchumi ili ipate fursa ya kushiriki kikamilifu katika kujitafutia maendeleo," alisema. 

Alitaja mambo mengine kuwa ni pamoja na kusisitiza kuongeza ajira kwa vijana, kuhamasisha masuala ya afya na maendeleo kwa wanawake, watoto pamoja na kuongeza kasi ya biashara ya kikanda. Alisema pia katika mkutano huo wanatarajia kujadili namna ambavyo nchi ya Burundi inaweza kuruhusiwa kujiunga kuwa mwanachama wa SADC. 

Awali, akizungumza aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, Ndaitwah, alitoa pole kwa serikali na kueleza  kusikitishwa kwa ajali ya mlipuko wa lori la mafuta mkoani Morogoro iliyosababisha vifo  vya watu zaidi ya 75 na wengine kadhaa kujeruhiwa kwa moto.

 

Alisema yeye ni mwenyeji nchini kwa kuwa anakumbuka  ameishi miaka ya 1980 na alijulikana kwa jina la 'Mama Swapo' hivyo kuwa Dar es Salaam anajiona kama yupo nyumbani kwake.

Alisema anashukuru kwa hatua zilizofikiwa katika  kutekeleza malengo ya mkutano wa 38, ambao ulikusudia kuangalia maboresho na ujenzi wa miundombinu na uwezeshaji wa vijana. 

 Alieleza jinsi ambavyo SADC inashukuru uchaguzi uliofanyika katika nchi sita ambazo ni ESwatini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jamhuri ya Madagascar, Muungano wa Comoros, Malawi na Afrika Kusini.

"Nazipongeza serikali na wananchi katika nchi nilizotaja  kutokana na kufuata misingi ya demokrasia na kumaliza uchaguzi kwa amani," alisema.

Habari Kubwa