Kanisa lavunjwa  kwa amri ya DC

14Aug 2019
Beatrice Moses
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kanisa lavunjwa  kwa amri ya DC

KANISA la EAGT katika Kijiji cha Lwang'a, Kata ya Kasanga wilayani Mufundi, limevunjwa kwa amri ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Jamhuri William.

Imedaiwa kuwa kanisa hilo lilijengwa kwa mabanzi likigharimu Sh. milioni 2.5 na lilianza kutumika Machi 27, mwaka huu.

Mmoja wa wazee wa kanisa hilo, aliyeomba hifadhi ya jina lake, alisema wamefadhaishwa na hatua hiyo kwa kuwa wamekosa mahali pa kuabudu.

Alidai eneo lilikokuwa limejengwa kanisa hilo, walilinunua Machi 20, mwaka huu kwa Sh. 500,000.

Mkuu wa Wilaya hiyo (William), aliliambia Nipashe juzi kuwa amelazimika kuchukua hatua hiyo kwa sababu za kiusalama, akieleza kuwa amekuwa akiwafuatilia kwa karibu wahusika wa kanisa hilo na kubaini ni 'waasi'.

Kiongozi huyo wa serikali alikiri kuamuru jengo hilo la kanisa livunjwe kwa kuwa lilijengwa bila kibali cha serikali.

"Mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, nilijiridhisha kwamba kikundi hicho kilikuwa ni cha waasi waliokuwa wamekusudia kuvuruga amani.

"Ndiyo maana niliamuru jengo lile livunjwe, siamini kama lilikuwa kanisa maana halikusajiliwa," alisema.

Aliongeza kuwa uanzishwaji wa makanisa una utaratibu wake ambao upo kwa mujibu wa sheria, hivyo kila anayeanzisha huduma hiyo anapaswa kuuzingatia.

"Wamefanya majaribio kadhaa ili kuhujumu kanisa walilokuwa wakisali awali ikiwamo kutaka kulilipua, pia walikwenda kuvuna msitu, watu watatu wamekamatwa na wiki hii watapandishwa kizimbani," alisema.

Nipashe imebaini Mchungaji Mwakosya wa kanisa hilo aliandikiwa barua na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mufindi Agosti 5, mwaka huu, akitakiwa kuwasilisha nyaraka za usajili wa kanisa.

Barua hiyo ambayo ilitiwa saini na Mkuu wa Wilaya hiyo (William), akimtaka mchungaji huyo kuwasilisha nyaraka za usajili wa kanisa hilo saa tatu asubuhi Jumanne Agosti 6, mwaka huu bila kukosa.

Mchungaji Mwakosya wa kanisa hilo aliliambia Nipashe kuwa hakutekeleza agizo la Mkuu wa Wilaya na ilipofika saa sita mchana, watu walivamia kanisani na kulivunja.

Mchungaji huyo alidai anaamini hatua hiyo imechukuliwa kutokana na mgogoro ulioko kwenye ngazi ya kitaifa ya uongozi wa Kanisa la EAGT.

Alidai kanisa hilo ni tawi la Kanisa la EAGT, hivyo limesajiliwa, na viongozi wake akiwamo yeye wanafanya shughuli zao kihalali na wana vitambulisho vya kazi. 

Habari Kubwa