Tani 20 pamba zakamatwa zikisafirishwa kwa magendo

14Aug 2019
Happy Severine
BARIADI
Nipashe
Tani 20 pamba zakamatwa zikisafirishwa kwa magendo

GALI lenye zaidi ya tani 20 za pamba iliyonunuliwa kwa magendo na baadaye kusafirishwa bila kufuata utaratibu, limekamatwa katika Kata ya Dutwa wilayani Bariadi mkoani Simiyu.

Imeelezwa kuwa gari hilo lenye namba za usajili T 917 BCN lilikamatwa juzi saa nne usiku likiwa limepakia iliyokuwa imekusanywa  nyumbani kwa mtu katika Kata ya Gilya wilayani hapa kinyume na utaratibu.

Kwa mujibu wa utaratibu, pamba yote inatakiwa kununuliwa kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS).

Akizungumza katika eneo la tukio jana,  Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, aliagiza gari hilo pamoja na dereva kushikiliwa na Jeshi la Polisi mpaka  wanunuzi wa pamba hiyo watakaposakwa na kupatikana.

"Ninaliagiza Jeshi la Polisi kuendelea kulishikilia gari hilo pamoja na dereva, huku wakiwasaka wanunuzi wa pamba hiyo watafutwe ili waje kujibu kosa hilo la kununua na kusafirisha kimagendo,” alisema Kiswaga na kuwaagiza wanunuzi hao wajitokeze mara moja na kujisalimisha wenyewe.

Dereva wa gari hilo, Lulyalya Deus, alieleza kutowafahamu wanunuzi wa pamba akidai kuwa yeye alilipwa malipo ya kazi ya kusafirisha.

Kadhalika, alikiri kushuhudia pamba hiyo kuanzia inapopakiwa kwenye gari, na kwamba watu hao walitoroka wakati gari liliposimamishwa kwa ajili ya ukaguzi.

Katika kukabiliana na wizi wa pamba wilaya humo, Kiswaga amewataka watendaji wa mitaa na kata kuwa walinzi katika maeneo yao, na kuhakikisha hakuna pamba inayonunuliwa bila kufuata utaratibu.

Habari Kubwa