Anayedaiwa kuua mke atishia kuwafanya kitu kibaya waandishi

14Aug 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Anayedaiwa kuua mke atishia kuwafanya kitu kibaya waandishi

MSHTAKIWA Khamis Luwonga maarufu kwa jina la Meshack (38), anayetuhumiwa kumuua mkewe kwa kumchoma moto ameiambia mahakama kuwa atakuja kuwafanyia kitu kibaya waandishi wa habari wanaompiga picha.

Kadhalika, amedai atawafanyia kitu kibaya ambacho mahakama hiyo, haitatarajia kwa kuwa ameshachanganyikiwa na hajui mtoto wake yuko wapi, hivyo anahitaji amani ya moyo.

Mshtakiwa huyo alitoa madai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Salum Ally, jana kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya kutajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.

Mshtakiwa huyo aliomba ruhusa ya kuongea mahakamani na hakimu na alipomkubalia alidai kuwa anakerwa na waandishi wa habari kumpiga picha na kwamba ameshachanganyikiwa kwa kuwa hajui mtoto wake alipo.

"Mheshimiwa nina kitu ambacho nataka nikueleze kuhusu waandishi wa habari, wamekuwa wakinipiga picha kuanzia chini hadi ndani ya mahakama, sasa nakueleza hivi nitakuja kuishangaza mahakama nitafanya kitu kibaya sana, ninakabiliwa na kesi na sielewi hatima yangu, hapa nilipo kichwa changu kimevurugika, nina mawazo ya mtoto wangu na ninapofika hapa ili akili yangu itulie, wanakuja kunipiga picha sasa nawaeleza kuwa nitafanya kitu kibaya ambacho mahakama haitatarajia," alidai Luwongo.

Kufuatia kauli hiyo ya vitisho kwa waandishi wa habari, Wakili Wankyo alimweleza mshtakiwa kuwa, kupigwa picha ni hali ya kawaida kwa mshtakiwa yeyote anayefikishwa mahakamani, wote wanapigwa picha, hivyo amemtaka awape uhuru waandishi wa habari wafanye kazi yao.

Hakimu aliamuru mshtakiwa arudishwe rumande na kesi hiyo itatajwa Agosti 27, mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Katika kesi hiyo, mshtakiwa anatuhumiwa kwa kosa moja la mauaji kinyume cha sheria ya kanuni ya adhabu namba 196 sura 16, kama kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Katika kesi hiyo, mshtakiwa Luwonga ambaye ni mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam anadaiwa Mei 15, 2019 akiwa Gezaulole eneo la Kigamboni, alimuua Naomi Marijani.

Mwanzoni mwa mwezi Julai, mwaka huu, mshtakiwa Meshack alisambaza tangazo magazetini na kwenye mitandao ya kijamii kuwa anamtafuta mke wake ambaye alitoweka ghafla, lakini baadaye Jeshi la Polisi kupitia Mkuu wa Upepelezi wa kanda hiyo, Camillius Wambura, alitangaza kumshikilia Luwonga akidaiwa kumuua na kisha aliuchoma moto mwili wa mkewe.

Habari Kubwa