Mashine ya ‘utra sound’ yaibwa hospitalini

14Aug 2019
Happy Severine
BARIADI
Nipashe
Mashine ya ‘utra sound’ yaibwa hospitalini

KATIKA hali ya kushangaza mashine inayotumika kupima magonjwa kutambua taarifa mbalimbali katika mwili wa binadamu (utra sound) imeibwa na watu wasiojulikana kwenye wodi mpya ya wajawazito Hospitali ya Wilaya ya Bariadi.

utra sound

Mashine hiyo pamoja na kifaa chake cha kudurufu karatasi (printer) na nyaya zake zote viliibwa Agosti 5, mwaka huu, majira ya mchana na mpaka sasa havijapatikana.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake, Mganga Mkuu wa halmashauri hiyo, Mike Mabimbi, alikiri kuibwa kwa mashine hiyo Agosti 5, mwaka huu.

Mabimbi alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo walitoa taarifa polisi na watu 17 wakiwamo wauguzi walikamatwa kwa ajili ya mahojiano.

"Ni kweli mashine hiyo ambayo ilitolewa na wadau wa maendeleo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), kwa ajili ya wodi ya kinamama pekee iliibiwa katika mazingira ya kutatanisha, tayari taarifa tulitoa polisi na wanaendelea na uchunguzi," alisema Mabimbi.

Aliongeza kuwa mashine hiyo inafanana na kompyuta mpakato (laptop), hivyo mtu yeyote mwenye nia ovu alikuwa na uwezo wa kuiba na kuweka kwenye begi na kutoweka nayo.

"Mashine hiyo ilitolewa kwa ajili ya wajawazito tu na ilikuwa humo kwenye wodi kwa ajili ya kurahisisha huduma na wodi hiyo, ilikuwa na vifaa vyote vinavyohitajika kwa mjamzito kikiwamo chumba cha upasuaji," alisema Mabimbi.

Alisema baada ya kuibwa kwa kifaa hicho wanalazimika kuwapeleka wajawazito kwenye mashine kama hiyo kubwa iliyoko chumba cha mionzi takribani mita 10 kutoka kwenye wodi hiyo na kueleza kuwa inasababisha usumbufu.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Mwanaidi Churu, alisema mazingira ya kuibwa kwa kifaa hicho yameendelea kuwa magumu kutokana na watoa huduma kwenye wodi hiyo kuwapo na kila mmoja kudai hajui.

Alisema baada ya mashine hiyo kuibwa wafanyakazi hao waliitwa na waliokuwa zamu usiku hadi asubuhi walieleza kuwa kifaa walikiacha, lakini walioingia mchana walidai kutokikuta.

"Kila siku hapa hospitali ni vikao na bado kifaa hakijapatikana, ingawa huduma zinaendelea, lakini kuna usumbufu maana kile kilikuwa humo humo ndani," alisema Churu.

Viongozi hao waliwaomba wananchi kutoa taarifa kwa polisi au kwa kiongozi wa serikali yeyote atakayeona kifaa kama hicho kinauzwa.

"Kifaa hiki kimeletwa hapa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wajawazito ambaye ameiba hakiwezi kumsaidia chochote, tunaomba waandishi wa habari na wananchi mtusaidie katika kupatikana kwa kifaa hiki ni muhimu sana," alisema Mabimbi.

Habari Kubwa