Malinzi aeleza   TFF ilivyodaiwa

14Aug 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Malinzi aeleza   TFF ilivyodaiwa

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (59), amedai mahakamani kuwa wakati anaingia madarakani shirikisho hilo lilikuwa na hali ngumu kiuchumi iliyosababisha madeni makubwa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kusababisha akaunti zake kufungwa kila wakati.

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (59)

Malinzi alitoa madai hayo jana wakati akijitetea dhidi ya mashtaka ya kughushi na kutakatisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Richard Rweyongeza, Malinzi alidai hali hiyo ilikuwa ikimlazimu kuikopesha TFF fedha zake binafsi na alikuwa akifanya hivyo kupitia akaunti waliyoifungua kati yake na shirikisho hilo.

Malinzi alidai kuikopesha TFF kutokana na hali ngumu ya kifedha iliyokuwa ikiikabili na hivyo kulazimika kutumia fedha zake binafsi, kukopa kwa watu binafsi ama kamati ya utendaji ili kunusuru hali hiyo hasa katika matukio muhimu yanayoikuta TFF na timu ya Taifa Stars.

Akitaja baadhi ya matukio ambayo alilazimika kutoa fedha zake na kuikopesha TFF, ni kuilipa Kampuni ya Pachi Line iliyokuwa ikitoa huduma za tiketi ambayo iliwahi kukamata basi la shirikisho hilo kupitia hati waliyopewa mahakamani, lakini ili kunusuru hilo alilazimika kutoa fedha zake kuilipa kampuni hiyo.

Tukio lingine ni kuilipa Sh. milioni 20 kampuni ya udalali ya Yono, ambazo TFF ilikuwa ikidaiwa na walitaka kukamata basi la shirikisho hilo ambalo lilitolewa na wafadhili ambao walikuwa kampuni ya bia (TBL), pia alilipia Sh. milioni 40 za tiketi za ndege Kampuni ya Ethiopia Airline za wachezaji wa Taifa Stars, waliokuwa wanakwenda nchini Nigeria katika mashindano ya Afrika.

"Mheshimiwa mimi niliwahi kuikopesha TFF Dola za Kimarekani 7,000 nikiwa Harare, Zimbabwe baada ya wachezaji wa Taifa Stars kutolewa mizigo yao nje ya hoteli tuliyofikia kwa sababu shirikisho la mpira Zimbabwe lilikuwa likidaiwa na hoteli hiyo, hata baadhi ya mashahidi waliowahi kutoa ushahidi wao hapa mahakamani walithibitisha hilo akiwamo Kaimu Mkurugenzi wa Fedha wa TFF, Daniel Maangi," alidai Malinzi.

Alidai deni la mwisho analokumbuka kuikopesha TFF ni Sh. milioni 15 alizolipa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ili wakalipie Kampuni ya Azam mwaka 2017, ikiwa ni takwa la mfadhili Kampuni ya Serengeti kutaka mechi za Taifa Stars zionyeshe bure na Taifa Stars ilikuwa ikicheza dhidi ya Lesotho.

Alidai wakati anaingia madarakani alikuta shirikisho hilo likiwa na madeni makubwa kutoka TRA na hiyo ilisababisha TFF kufungiwa akaunti zake mara kwa mara na wakati mwingine kuletewa hati za kuitwa mahakamani.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 15, mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi wa nyaraka za taarifa ya madeni kati ya Malinzi na TFF.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, Karani Flora Rauya na Selestine Mwesigwa.

Habari Kubwa