Waziri ataka Watanzania kujisajili

14Aug 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waziri ataka Watanzania kujisajili

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Balozi Dk. Augustine Mahiga, amewataka wananchi kujisajili na kuwa na vyeti vya matukio muhimu ya kibinadamu kama vyeti vya kuzaliwa, vifo, ndoa na talaka.

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Balozi Dk. Augustine Mahiga

Waziri Mahiga alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa maadhimisho ya pili ya Siku ya Usajili wa Matukio Muhimu kwa Binadamu na Takwimu Barani Afrika yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema usajili wa matukio muhimu ni suala ambalo linafanyika duniani kote na ni muhimu kwa mujibu wa sheria.

"Usajili ulikuwapo tangu enzi za ukoloni japo kulikuwa hakuna mfumo wa sheria, kwa sasa mfumo huo upo, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kujisajili ili taarifa zake zihifadhiwe," Mahiga alisema.

"Nimefurahi kwa maboresho ambayo yamekuwa yakifanywa na Rita (Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini) hasa kuhusisha na masuala ya teknolojia kwani kwa sasa dunia ipo katika mfumo wa kidigitali."

Balozi Mahiga pia aliwataka viongozi wa dini kuweka sawa taarifa za vyeti vya matukio ambayo ni vya kuzaliwa, kifo, ndoa na talaka ili kuisaidia serikali pindi zinapohitaji.

"Zamani tulikuwa tunahifadhi taarifa kama hizi kwa viongozi wa dini na ukienda kutaka kupata taarifa, unapata hadi za babu wa babu yako, kuanzia mwaka aliozaliwa, aliokufa na taarifa za familia yake, hili ni jambo muhimu sana kwa viongozi wetu wa dini," Balozi Mahiga alisema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson, alisema kuwa katika kuadhimisha siku hiyo, wametoa huduma za usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa bure kama mchango katika jamii kwa wanafunzi 150 wa Shule ya Sekondari Wama Nakayama, iliyoko wilayani Kibiti mkoani Pwani na wanafunzi 102 wa Shule ya Sekondari ya Wama Sharaf iliyoko wilayani Lindi.

Habari Kubwa