Simba SC na siri Caf, rekodi shida Yanga

14Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba SC na siri Caf, rekodi shida Yanga
  • *** Kila mtu na ashinde kwao yazidi kuwabeba Wekundu wa Msimbazi, rekodi mechi za ugenini kwa Wanajangwani tatizo kubwa...

WAKATI miamba ya soka nchini kwa sasa ikiwa katika maandalizi makubwa kuelekea mechi zao za marudiano za Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kulazimishwa sare kwenye mechi za awali, rekodi ya Simba kushinda nyumbani inaibeba huku watani zao, Yanga rekodi ya kupoteza ugenini ikionekana kufifisha-

-matumaini yao ya kusonga mbele.

 Simba itakuwa nyumbani Uwanja wa Taifa, Agosti 25 kuikaribisha UD Songo ya Msumbiji baada ya timu hizo kutoka sare tasa katika mechi ya awali iliyopigwa mjini Beira nchini humo, wakati Yanga iliyolazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Township Rollers, Agosti 24 itakuwa mjini Gaborone kurudiana na mabingwa hao wa Botswana.

Hata hivyo, Yanga ambayo ipo mkoani Kilimanjaro ikijiwinda na mechi hiyo ya marudiano, hofu imetanda kwa mashabiki wake kutokana na rekodi zake katika mechi za kimataifa hususan ikiwa ugenini.

 

Yanga Kimataifa

Kwa mujibu wa takwimu za Nipashe ambazo zinalandana kabisa na zile za Shirikisho la Soka Afrika (Caf), mwaka jana kabla ya michuano hiyo kuanza kuchezwa kwa mfumo wa msimu, kwenye michuano ya kimataifa ambayo Yanga iliiwakilisha nchi katika Ligi ya Mabingwa kabla ya kutolewa na kuangukia Kombe la Shirikisho, ilicheza jumla ya mechi sita ugenini na haikushinda hata moja, huku ikipoteza nne na kuambulia sare mbili tu.

Msimu huo katika hatua ya awali kabisa ya Ligi ya Mabingwa Februari 10, mwaka jana ilianzia nyumbani dhidi ya Saint Louis Suns United ya Shelisheli na kushinda bao 1-0 kabla ya siku 11 baadaye kupata sare ya bao 1-1 ugenini.

Mechi ya raundi ya kwanza Machi 6, mwaka jana ikaikaribisha Township Rollers katika Uwanja wa Taifa na kukubali kipigo cha mabao 2-1 kabla ya siku 11 baadaye kuifuata Botswana na kulazimisha sare ya bao 1-1, hivyo mabingwa hao wa Botswana kufuzu hatua ya makundi na Wanajangwani kuangukia mechi ya mchujo kusaka nafasi ya kucheza hatua ya makundi Kombe la Shirikisho.

Katika mechi ya mchujo, Yanga ilipangwa na Welayta Dicha ya Ethiopia ambapo ikiwa Uwanja wa Taifa Aprili 7, mwaka jana ilishinda 2-0 kabla ya siku 11 baadaye kukubali kipigo cha bao 1-0 ugenini.

Matokeo hayo yaliipeleka Yanga hatua ya makundi kwenye Kombe la Shirikisho ambapo iliangukia Kundi D ikipangwa sambamba na USM Alger ya Algeria, Rayon Sports ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya.

Katika hatua hii, Yanga ilianza kwa kipigo cha mabao 4-0 ugenini Algeria dhidi ya USM Alger Mei 5, kabla ya siku 11 baadaye kutoka sare tasa dhidi ya Rayon Sports Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Julai 18, mwaka jana ikaifuata Gor Mahia nchini Kenya na kulala 4-0 kabla ya siku 11 baadaye kurudiana Uwanja wa Taifa na kupigwa tena 3-2. Baada ya mchezo huo, Yanga iliialika USM Alger Uwanja wa Taifa na kushinda 2-1 Agosti 18, kabla ya siku 11 kwenda kulala kwa bao 1-0 ugenini Rwanda dhidi ya  Rayon Sports.

Matokeo hayo yaliifanya Yanga kumaliza mkiani mwa kundi bila kushinda mechi hata moja ugenini huku ikiwa na pointi nne tu, wakati UMS Alger iliyomaliza nafasi ya kwanza na Royon Sports ikimaliza nafasi ya pili zikifuzu hatua ya robo fainali.

Hata hivyo, Yanga haikuwa chini ya kocha wake mkuu wa sasa, Mwinyi Zahera ambaye tangu atue amekuwa lulu kwa mashabiki huku akijaribu kuisuka upya, hivyo anaweza kuwa mbeleko mpya kwa Wanajangwani hao katika mechi za ugenini.

Tayari Zahera amesema: "Kuna mambo yakufanyia marekebisho hususan safu ya ushambuliaji kutokuwa na muunganiko mzuri, katika mechi hizi za Caf ni muhimu sana kupata matokeo nyumbani.

"Lakini bado tunaweza kuingiza bao ugenini na hata kupata matokeo ya 2-1, hivyo tunajipanga kucheza kwa kasi mechi ya marudiano ugenini."

 

SIMBA KIMATAIFA

Mwaka jana Caf ilibadili mfumo wake wa michuano hiyo na kuanza kuandaliwa kwa mtindo wa msimu, ambapo msimu wa 2018/19, Simba waliipeperusha bendera nchi kwenye Ligi ya Mabingwa na kufanikiwa kutinga robo fainali.

Simba ambayo ilikuwa ikitamba na kaulimbiu yake "Kila mtu ashinde nyumbani", ilifanya vizuri kiasi ugenini kwenye mechi za awali na raundi ya kwanza, lakini hatua ya makundi ilikuwa na rekodi mbaya.

Simba ilianza hatua ya awali kwa kushinda mabao 4-1 nyumbani dhidi ya Mbabane Swallows ya Eswatini (zamani Sawaziland) kabla ya kuifuata kwao na kuichapa 4-0.

Mechi iliyofuata ikachapwa 2-1 ugenini Zambia dhidi ya Nkana FC, kabla ya kuifumua mabao 3-1 kweye Uwanja wa Taifa na kufanikiwa kutinga hatua ya makundi ambapo changamoto ya kupoteza ugenini ilianzia hapo.

Hatua ya makundi ilianzia nyumbani kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Saoura ya Algeria kabla ya kwenda DR Congo na kunyukwa mabao 5-0 dhidi ya AS Vita kipigo kama hicho ikikipata pia ilipoifuata Al Ahly nchini Misri, lakini pia ilipoifuata JS Saoura ikatandikwa 2-0, hivyo kujikuta ikishindwa hata kupata sare ikiwa nje ya Uwanja wa Taifa katika hatua hii.

Hata hivyo, ilifanikiwa kushinda bao 1-0 Uwanja wa Taifa dhidi ya Al Ahly na  2-1 dhidi ya AS Vita na kuweka rekodi ya kushinda mechi zake zote za nyumbani hatua ya awali, raundi ya kwanza na hatua ya makundi.

Hatua ya robo fainali Simba ikalazimishwa sare tasa dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, ikiwa ni mara yake ya kwanza kukosa ushindi katika Uwanja wa Taifa kwa msimu huo, kabla ya kwenda kutolewa ugenini kwa mabao 4-1.

Hivyo, matokeo ya sare tasa kwa Simba ugenini yanaipa matumaini makubwa ya kushinda nyumbani ambapo imekuwa ikipata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wake.

Tayari Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, amesema ana uhakika wa kufanya vizuri nyumbani dhidi ya UD Songo na kusonga mbele.

"Kikubwa tumeweza kuzuia na kutoruhusu bao ugenini, nina uhakika tunaweza kufanya vizuri mechi ya marudiano nyumbani na kusonga mbele," alisema Aussems.

Habari Kubwa