BAADA YA MIAKA 55

14Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
BAADA YA MIAKA 55
  • Pius Msekwa aeleza misumari ya siri iliyoshikilia Muungano-9

PIUS Msekwa (84), ni miongoni mwa wakongwe waliobeba wasifu mkubwa katika kulitumikia taifa, ikiwamo kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)-

-na Katibu Mtendaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), pia mshauri muhimu wa Serikali na chama (TANU na CCM) kwa mengi.

Pia Msekwa ana sifa nyingine ya kipekee, kuwa mdau anayefahamu fika picha kamili ya dhana ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao mzizi wake kwa hatua, wengi hawaufahamu kwa kina kutokana na umri na si yote yaliyokuwa bayana.

Ili kuliweka hilo wazi kwa kina tangu vuguvugu na kuundwa Muungano huo, ameamua kuandika kitabu alichokizindua siku chache zilizopita, kiitwacho Historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kinachoweka undani wa historia kwa hatua. Gazeti hili limeamua kuchapisha maudhui yake kwa hatua, kila siku kama ya leo katika jarida hili la Siasa na leo hii tunaendelea kutokea tulipoishia wiki iliyopita. Endelea na sehemu hii ya tisa ya kitabu hicho inayoanzia na ‘Kuhusu Madai ya Tume ya Nyalali’…

 (ii) Kuhusu madai ya Tume ya Nyalali

Mwalimu Nyerere aliyapuuzilia mbali kwa maneno aliyoyaandika katika kitabu chake kiitwacho “Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania:”

  • “Lakini, ukweli wa jambo hili unabaki palepale. Wananchi wa Tanzania hawadai serikali ya Tanganyika. Na mimi nasema, ukifufua Tanganyika, utaua Tanzania. Fahari wawili hawakai zizi moja. ‘Yeltsin’ wa Tanganyika ataua Muungano.

 

(ii) Kuhusu madai ya Azimio la Bunge la kutaka iundwe serikali ya Tanganyika

Nguvu kubwa ya Mwalimu Nyerere katika kupinga muundo wa serikali tatu ilidhihirika katika jitihada zake za kupinga Azimio la Bunge la kutaka serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano. Madai hayo yaliibuliwa wakati Mwalimu Nyerere alipokuwa tayari amekwishakustaafu Uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi. Lakini, bado aliweza kutumia nguvu kubwa na uwezo wake mkubwa aliokuwa nao wa kushawishi watu, katika kupinga azimio hilo la Bunge. Alifanya hivyo katika vikao vyake vya faragha na viongozi wakuu wa chama na serikali ngazi ya taifa, alifanya hivyo katika vikao vya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ambavyo alihudhuria kwa kualikwa, na alifanya hivyo hadharani katika mkutano wake na waandishi wa habari. Kwa sababu hakuwa madarakani, haikuwa rahisi kwake kupata mafanikio. Kitabu chake cha “Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania” kinaeleza kwa kirefu jinsi alivyovunjwa moyo kutokana na Wakuu wa Chama na Serikali kutokuthamini ushauri wake kwao.

Hatimaye, alipochoshwa na usugu wa viongozi hao wa kutokuwa tayari kukubali ushauri wake, Mwalimu Nyerere aliamua kuelekeza mashambulizi yake kwa viongozi hao, yaani, Rais Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu John Malechela na Katibu Mkuu wa Chama, Horace Kolimba.

Mwalimu aliandika hivi katika kitabu chake cha ‘Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania’:

  • “Washauri wake (Rais Mwinyi) walipomshauri akubali hoja ya kufufua Tanganyika na kuipatia serikali yake, badala ya kukataa na kumfukuza Waziri Mkuu, Rais wetu alikubali! Alifanya hivyo akijua athari za kufufua Utanganyika, na baada ya yeye mwenyewe kusimama mbele ya wabunge siku chache tu zilizopita na kupinga hoja ya serikali tatu.”

 

Hatimaye, mnamo mwezi Desemba 1994, Rais Mwinyi alimwondoa madarakani Waziri Mkuu John Malechela na kumteua Cleopa Msuya kushika nafasi hiyo; na pia alimwondoa madarakani Katibu Mkuu wa Chama Horace Kolimba na kumteua Lawrence Gama kushika nafasi hiyo.

(iv)  Kuhusu Madai ya Tume ya Jaji Kisanga

Mwalimu Nyerere hakupata nafasi ya kupinga pendekezo la serikali tatu ambalo lilitolewa na Tume ya Jaji Kisanga, kwa sababu taarifa ya tume hiyo iliwasilishwa kwa Rais Benjamin Mkapa kwa barua liyoandikwa tarehe 20 Agosti, 1999, wakati ambapo Mwalimu Nyerere alikuwa ameanza kusumbuliwa na maradhi ambayo hatimaye yalimwondoa duniani mwezi Oktoba mwaka huohuo.

6.4     Majadiliano katika Bunge Maalum la Katiba

Majadiliano yalivyokuwa katika Bunge Maalum la Katiba yaliweka wazi sababu zinazotolewa na wale wanaodai muundo wa serikali tatu na sababu zinazotolewa na watetezi wa muundo wa serikali mbili. Kwa hakika, hii ilikuwa chemsha bongo ya aina yake.

Uchambuzi unaonesha kwamba sababu kubwa kwa pande zote mbili ni kuzuia Muungano usivunjike. Kila upande ulikuwa unadai kuwa, muundo wa Muungano wanaoutetea wao, ndio utakaookoa Muungano usivunjike. Hii ni chemsha bongo ya aina yake, kwani siyo rahisi kuelewa kwamba, pande mbili zinazotetea miundo tofauti kabisa, eti zinakuwa na lengo lilelile moja la kuokoa Muungano usivunjike!

Tuliweza kuisikia chemshabongo hii katika mjadala uliokuwa ukiendelea katika Bunge Maalum la Katiba (2013), na jinsi kila upande ulivyokuwa ukitetea hoja zake kwa nguvu kubwa. Hatuna haja ya kurudia kuzitaja hoja zote hizo hapa. Lakini, kwa muhtasari, zilikuwa kama ifuatavyo:

  • Watetezi wa serikali mbili walidai kwamba, muundo huu umekuwapo kwa miaka hamsini iliyopita. Matatizo mengi yaliyojitokeza yameweza kutatuliwa, na kero nyingi zimeondolewa. Wanadai kwamba, muundo wa serikali tatu utaleta mzozo mkubwa baina ya Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar katika suala la kuchangia fedha za kuendesha Serikali ya Muungano. Kwa kuwa Zanzibar haina uwezo wa kuchangia kiasi kikubwa, katika muundo wa serikali tatu, Tanganyika nayo itakataa kubeba mzigo huo peke yake, na mzozo huo lazima utasababisha kuvunjika kwa Muungano.
  • Kwa upande wao, wale wanaodai muundo wa serikali tatu walidai kwamba, muundo wa serikali mbili umesababisha kuwapo kwa malalamiko na kero nyingi kwa pande zote mbili za Muungano, kero ambazo zimeshindikana kutatuliwa kwa muda mrefu wa miaka hamsini iliyopita. Wanaendelea kudai kwamba, hatimaye, malalamiko haya yatazaa hasira kali ambazo zitasababisha kuvunjika kwa Muungano. Lakini, katika muundo wa Serikali tatu, kila upande utakuwa na Serikali yake, ambazo zitakuwa zikishauriana katika hali ya usawa juu ya namna ya kutatua matatizo yoyote yatakayokuwa yanajitokeza. Hali hiyo ya usawa ndiyo itakayoimarisha Muungano na kuzuia usivunjike.

Lakini, zaidi ya hayo ni kwamba, kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika kutaiondoa Tanganyika katika hali ya kuwa ‘imevaa koti la Muungano’, na kudhihirisha usawa baina ya nchi mbili zilizoungana.

6.5 Hoja ya kutetea Muundo wa Serikali mbili

Pamoja na sababu zilizotolewa katika Bunge Maalum la Katiba za kutetea muundo wa Muungano wa serikali mbili, ni vizuri vilevile kujielekeza kwenye sababu halisi zilizowafanya waasisi wa Muungano kuweka muundo huo, kwa kujikumbusha maelezo ya Mwalimu Nyerere kwamba, “Hatukutunga mfumo huu kama wapumbavu. Tulitazama hali yetu halisi ilivyokuwa, na tukabuni mfumo uliotufaa zaidi katika hali hiyo” na “hali halisi” iliyozingatiwa wakati huo ilikuwa ni ‘udogo wa Zanzibar na ukubwa wa Tanganyika’; kwa maana idadi ya watu wa kila upande. Swali muhimu hapa ni je, hali hiyo sasa imebadilika? Jibu lake ni dhahiri kabisa kwamba hali hiyo bado haijabadilika. Kwa hiyo, mantiki ya muundo wa serikali mbili bado iko palepale.

6.5.1 Hofu kwamba, muundo wa serikali tatu utavunja Muungano

Kwa uchambuzi wangu: Idadi ya serikali siyo kinga dhidi ya Muungano kuvunjika. Idadi yoyote ya serikali, (ziwe ni mbili au ni tatu) siyo kinga ya uhakika ya kuzuia Muungano usivunjike, kwani upo uzoefu wa nchi nyingine zilizowahi kuungana, lakini, muungano wao ukavunjika bila kusababishwa na idadi ya serikali katika Muungano wao, mfano, Misri (Egypt) Syria, Senegali na Gambia.

6.5.2 Mifano ya Miungano iliyovunjika na sababu zake

Mfano mmoja ni ule wa nchi ya Egypt na Syria. Nchi hizo mbili ziliungana rasmi mwezi Februari 1958 na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu, iliyopewa jina la United Arab Republic (U.A.R.). Muungano huo ulidumu kwa kipindi cha miaka minne tu hadi Septemba 1961, ulipovunjika. Sababu ya kuvunjika kwake ni kujitoa kwa Syria kwenye Muungano huo baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea katika nchi hiyo.

Hapa tunaona kwamba, kilichosababisha kuvunjika kwa Muungano huo ni mabadiliko ya Serikali ya Syria, ambapo serikali ya kijeshi iliyotwaa madaraka huko haikuwa na utashi wa kisiasa wa kuendelea kubaki ndani ya Muungano huo.

Mfano mwingine ni nchi ya Senegali na Gambia, zilizoungana katika muundo wa ’Confederation” kuanzia tarahe 1 Februari, 1982, na kujulikana kwa jina la Senegambia. Muungano huo ulivunjika  tarehe  30 Septemba, 1989, siyo kwa sababu ya idadi ya Serikali katika muundo wao, bali ni kwa sababu ya utashi wa kisiasa wa nchi hizo na kubaki kwenye Muungano, ulitoweka.

Vilevile, kuna mfano wa “Central African Federation” iliyoundwa na wakoloni ikiunganisha nchi zilizokuwapo wakati huo za Southern Rhodesia, Northern Rhodesia na Nyasaland. Wapigania uhuru wa nchi hizo waliupinga sana muungano huo wa kulazimishwa na wakoloni, na walifanikiwa kuuvunja walipopata uhuru.

Sababu ya kuvunjika kwa Muungano huo ni kutokuwapo kwa utashi wa kisiasa wa viongozi walioshika madaraka katika nchi hizo baada ya uhuru…

Habari Kubwa