Mwaka unakatika, DRC waanza kujadiliana orodha ya mawaziri

14Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mwaka unakatika, DRC waanza kujadiliana orodha ya mawaziri

KIELELEZO cha msingi kuwa uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ulivurugwa na kutoa matokeo yasiyo sahihi ni kushindwa kwa Rais Felix Tshisekedi kuunda serikali tangu achaguliwe au atangazwe mshindi mwezi Januari mwaka huu.

Rais wa zamani wa DRC, Joseph Kabila (aliyenyoosha mkono), anadaiwa kuchangia ucheleweshaji wa kuundwa kwa Baraza la Mawaziri nchini humo.

Ilitazamiwa kuwa hadi Machi angekuwa ameunda serikali lakini alikwama kabisa, na hadi kufikia mwezi Mei akawa ameafikiana na rais aliyestaafu kidogo tu, Joseph Kabila, kuwa msaidizi wa karibu wa Kabila ndiye achukue nafasi ya uwaziri mkuu.

Mwishoni mwa Julai walikubaliana idadi ya mawaziri watakaokuwako serikalini, na wakati Agosti inaanza wanajadili majina ya mawaziri.

Taarifa kutoka Kinshasa zinaonyesha kuwa majadiliano ya kuunda serikali tangu mwanzo yanafanywa na Tshisekedi na Kabila moja kwa moja, siyo kupitia umoja wa upinzani na hata makundi ya vyama bungeni.

Ila mwafaka wowote unaopendekezwa lazima ufikishwe bungeni uthibitishwe, na ndiyo Tshisekedi alipoanza kukwama, kwani kundi la Kabila lina wabunge wengi.

Halafu isitoshe wabunge wa uliokuwa upinzani wakati wa Kabila wamegawanyika kutokana na kutangazwa Tshisekedi kuwa mshindi, badala ya Martin Fayulu aliyeonekana na makundi tofauti ya waangalizi wa kura ndani na nje ya DRC waliokuwapo kuwa alishinda.

Hali ya kushindwa kuunda serikali na mparaganyiko wa utii bungeni ambako kuna kambi kadhaa hasimu ni ushindi kwa Kabila ambaye ameondoka Ikulu, lakini hakuna kitu kilichobadilishwa hadi sasa, na saini yake inatakiwa ili chochote kifanyike.

Bila wabunge wake kumuunga mkono Tshisekedi, Rais anakuwa hana uwezo wa kupitisha chochote, wakati ambapo kuna kila ishara kuwa anazo hitilafu si ndogo siyo tu na Kabila mwenyewe bali zaidi tu na wasaidizi wake, hasa mawaziri waliokuwapo, au wanaoendelea kubakia hadi wengine watangazwe. 

Ingekuwa ni miaka ya zamani, jeshi tayari lingekuwa limeshapindua kuondoa mkwamo serikalini, si siku hizi.

Katika ishara kuwa Kabila anahakikisha anashika nchi kama mwanzo hata kama itachukua mwaka mzima kuunda serikali, taarifa zinasema kuwa amekazania kuwa kundi lake la wabunge litashika nafasi tatu kati ya nne za wizara muhimu zaidi, yaani ulinzi, fedha na sheria.

Ina maana wizara nyingine muhimu itakayokwenda kwa kundi la Tshisekedi ni mambo ya ndani na mambo ya nje, licha ya kuwa nafasi ya waziri mkuu pia itakwenda kwa kundi la Kabila.

Ni gharama kubwa ya kuvuliwa madaraka halisi ya urais kwa Tshisekedi, anayolipa kwa kupewa nafasi hiyo.

Nguvu kubwa ya Kabila inaonekana iko serikalini ambako ameisimamia kwa miaka 18 kama rais, hivyo ameteua wakuu wa taasisi zote nchini na watangulizi wao, ‘kuanzia vizazi vya tatu na vya nne.’

Kwa maana hiyo bila rais aliyechaguliwa kwa nguvu na wananchi, achukue madaraka kamili, haitakuwa rahisi kupangua ‘le systeme Kabila,’ kama ambavyo inaitwa kwa Kifaransa.

Isitoshe, akishateuliwa waziri mkuu itakuwa lazima kwa rais kumshirikisha kwa kila atakalotaka kufanya hasa katika kubadili washika madaraka maeneo tofauti, pale ambapo hawajafikia umri wa kustaafu, au pale anapotaka kutumia madaraka yake kuwastaafisha.

Na kama ilivyokuwa Sudan Kusini, katika muungano wa makundi yenye nguvu, upande wa kundi la mshindani-rais wanamsikiliza kiongozi wao, kwa maana hiyo Kabila, kwa uamuzi wowote ule; rais hawatishii…

Fununu zinasema kuwa Kabila ametaka pia wafuasi wake wapewe wadhifa wa wizara inayosimamia hisa za serikali, inayoshika kampuni za madini ambako kampuni kubwa ya shaba na ‘cobalt’ Gecamines, ina ubia na Glencore na Molybdenum ya China.

Pamoja na mambo ya nje na mambo ya ndani, bajeti na uchumi pia vitashikwa na kundi la Tshisekedi, ambao ina maana mgao wa ruzuku majimboni na sera za uwekezaji, wakati masuala ya fedha, benki na Benki Kuu, yanabaki chini ya kundi la Kabila.

Kundi la Kabila lilifurahia matokeo ya mazungumzo hayo na azma ya kuunda baraza jipya la mawaziri ambako ndio watakaotawala.

Jumla ya nafasi za uwaziri zinazotazamiwa ni 65, wakiwa ni 42 kutoka kundi la Kabila na 21 kutoka kundi la Tshisekedi, idadi ambayo inazidi ukubwa wa mabaraza ya mawaziri wakati wa Kabila.

Tayari Tshisekedi alishamtangaza Sylvestre Ilunga, swahiba wa Kabila kuwa waziri mkuu na makundi hayo mawili yakaunda umoja bungeni.

Tatizo limekuwa kutokana na hali ya kutokuaminiana kuhusu nani achukue wizara gani, kwani Tshisekedi amewahi kuwakosoa mawaziri wa Kabila kuwa wana tabia ya umila na ni wala rushwa, ina maana hana nia ya kuwatupa.

Mkwamo huo wa kuunda serikali na nguvu ya Kabila inayoonekana wazi imezua vurugu za hapa na pale lakini bado siyo za kina, kwani kuna shauku maeneo tofauti ya nchi nini ambacho serikali mpya inaweza kufanya.

Lakini historia inaonyesha kuwa mwelekeo wa kundi la Kabila hautabadilika na watataka wafanye watakavyo kwani bado ndio wenye wingi wa viti bungeni, na pande tofauti za upinzani hazielewani kutokana na ‘usaliti’ wa kukubali kuvuruga kura na kuteua mshindi asiye na wingi wa viti bungeni au idadi ya kura za wananchi.

Ina maana kuna uwezekano mkubwa wa serikali hiyo kushindwa kufanya kazi, au kukwama uchaguzi baadaye.

Inawezekana hali ya mkwamo ikaendelea kufukiwa fukiwa hadi uchaguzi mkuu miaka mitano baada ya ule wa Januari 2019, kwa sababu uwezekano wa ushindi wa Tshisekedi endapo akiamua kuitisha uchaguzi mwingine sasa, iwe ni kwa urais au kwa wabunge ni mdogo sana.

Itakuwa imeeleweka kuwa hakuwa mpinzani halisi bali mshirika msiri wa utawala ulioko madarakani.

Na isitoshe ushawishi wa wale waliovuna wakati wa Kabila utakuwa umepungua, pale wananchi watakapoelewa kuwa suala siyo kuwa na rais mwingine endapo hana wingi wa viti bungeni.

Ni kiashiria kuwa serikali ya Kabila kwa kivuli na ushirika wa Tshisekedi inaweza kudumu kwa miaka kadhaa kama itajitahidi, lakini inaweza kuvurugwa na maandamano ambayo hata sasa yanatokea lakini hayajashika kasi.

Ila kwa vile DRC ina tatizo la kuwepo kwa mwelekeo halisi wa kitaifa katika suala lolote lile, haitakuwa rahisi wananchi kujipanga nyuma ya Fayulu kama mgombea aliyepokonywa ushindi, kwani hata hivyo wingi wake wa viti bungeni ungesuasua.

Ila angeweza kuunda serikali na mojawapo ya makundi ya upinzani, hivyo tatizo ni kuwa licha ya ‘maandamano yasiyoisha’ wakati ule, wapigakura wa DRC walikuwa bado hawajaiva kuchagua serikali mpya kwa maana ya rais pamoja na wabunge.

Kabila ana viti vingi bungeni, hali halisi inayomwezesha apokonye au aelekeze nini kifanyike katika ngazi ya urais, kwani haina mizizi.

Habari Kubwa