Ni muhimu Waziri Lukuvi akalindwa

14Aug 2019
Salome Kitomari
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ni muhimu Waziri Lukuvi akalindwa

UPO usemi usemao mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Msemo huu hauna ubishi kwa Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kwani ni miongoni mwa viongozi walioweza kidhati kusimamia maeneo waliokabidhiwa.

Kila nikifungua mitandao ya kijamii na hasa YouTube nakutana na video za Lukuvi akifafanua mambo mbalimbali ya ardhi yanayogusa maisha ya watu, hasa walioporwa haki zao na wenye nguvu ya kifedha na mamlaka.

Kwa muda mrefu, ardhi imekuwa ni sekta iliyojaa dhuluma na uonevu hali iliyosababisha  watu kudai haki zao mahakamani na njia zingine walizoona zinastahili.

Dhuluma mojawapo ni mchezo mchafu baina ya madalali na taasisi za mikopo au watu binafsi ambao hukimbilia kuuza mali ya mtu na kubadilisha umiliki kwa haraka, huku wakimwacha mwingine katika maumivu makali.

Mathalani, wiki iliyopita vyombo vya habari vilitawaliwa na kisa cha mtu mmoja aliyeporwa haki yake kwa kuchukuliwa ghorofa lake na rafiki yake ambaye alishirikiana na watumishi wa idara ya ardhi kutengeneza hati ‘feki.’

Kama siyo Waziri Lukuvi ambaye ameamua kujitolea, hakika mtu huyo angekufa bila kurejeshewa mali yake hiyo.

Tukio jingine ni mkoani Arusha ambako kikongwe alinyang’anywa mali yake na kwa zaidi ya miaka 30 ameidai mahakamani bila kufanikiwa.

Lakini kwa sababu Waziri Lukuvi amejitoa sadaka, bibi huyo amerejeshewa mali yake.

Hakuna eneo gumu kama la ardhi ambalo limejaa wajanja wanaoshirikiana na baadhi ya madalali ambao miaka yote wamekula kwa jasho la watu, wakishirikiana na baadhi ya watumishi wa idara ya ardhi ambao huuza maeneo kwa zaidi ya mtu mmoja, wote wakipewa hati moja.

Hatua hii imesababisha waathirika kutumia gharama kubwa wakisaka haki zao kwenye mabaraza ya ardhi.

Hata hivyo imekuwa ngumu kupata haki kwa sababu walio kwenye mfumo ni watu ambao wanashirikiana na magenge ya ‘kijinai’ kunyanyasa raia.

Kwenye miji na majiji kuna kesi nyingi za watu kuporwa ardhi zao, wamiliki wawili kuwa na hati moja, na wengine kujeruhiwa au kufanyiwa ubaya licha ya kuwa ni haki yao.

Tangu aingie madarakani, siku zote Waziri Lukuvi amekuwa akitembea huku na kule kupambana na uhalifu huo na kimsingi amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuhakikisha wenye haki zao wanazipata.

Kwa sasa eneo la ardhi linaogopeka kufanya vinginevyo kwa sababu wajanja wanajua kwamba iwapo itajulikana, hatua zitachukuliwa dhidi ya mhusika.

Kila siku yanaibuka mapya katika eneo hilo na yote yamevaa sura ya uonevu dhidi ya watu, hasa wanyonge.

Na uonevu huu unapofuatiliwa kwa kina katika sekta hii ya ardhi ambayo ni muhimu sana kiuchumi, unakuta watu wenye nguvu ya fedha ambazo wamezitumia kujihalalishia maeneo hayo kinyemela.

Naamini waziri huyu akiendelea kuwapo katika kipindi chote cha awamu ya tano, Tanzania itapiga hatua kubwa katika suala zima la kumaliza migogoro ya ardhi ambayo mingi inatengenezwa kwa manufaa ya watu fulani.

Kwa kuwa mipango miji mingi ni ya zamani na ilipangwa kabla ya ongezeko la watu na mabadiliko makubwa ya kimaendeleo, ipo haja ya kufanyika kwa mipango mipya ya kupanga miji na majiji na hasa kwenye maeneo mapya ambayo bado hayajaendelezwa.

Kwa kazi kubwa anayofanya Waziri Lukuvi ni wazi kuwa amejitengenezea maadui ambao walipora haki za watu, na kwa kuwa wana fedha wanaweza kufanya lolote wakati wowote.

Kwa misingi hiyo ni vyema zikafanyika jitihada za kumlinda Waziri huyu kwa namna yoyote ili aendelee kutetea wanyonge ambao wameporwa haki zao.

Kikubwa kinachotakiwa ni kutenda haki kwa kila anayestahili pasipo kumwonea yeyote.

Habari Kubwa