Hali mbaya majeruhi ajali ya lori la mafuta

14Aug 2019
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hali mbaya majeruhi ajali ya lori la mafuta

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imesema majeruhi wanane kati ya 46 iliowapokea baada ya kujeruhiwa katika ajali ya lori la mafuta mkoani Morogoro, wamefariki dunia, huku 13 wakiwa kwenye hali mbaya.

Imesema majeruhi hao 13 wako kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) na wote wamepoteza ufahamu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika hospitali hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa MNH, Aminiel Aligaesha, alisema kati ya hao waliofariki dunia, mmoja aliongezeka jana.

"Tangu tumepokea majeruhi wa ajali hiyo, waliofariki dunia ni Jackson Shao, Kulwa Dominic, Ismail Mwanga, Muhidin Mtingwa, Maige Hamisi, Issa Musa, Adinandi Khamis na Amani Urio," alisema.

Aligaesha alisema wamekumbana na changamoto kutoka kwa ndugu wa majeruhi ambao wameshindwa kuwatambua ndugu zao kutokana na majeraha ya moto yaliyosababisha ugumu katika kuwatambua.

Alisema wameshirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya utambuzi wa wagonjwa kwa kutumia vipimo vya vinasaba (DNA).

Alibainisha kuwa kati ya majeruhi 39 wa ajali hiyo waliobaki katika hospitali hiyo kubwa zaidi nchini, 25 wamepata ufahamu na 13 bado wako katika hali mbaya.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Meneja wa Maabara ya Vinasaba kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Hadija Mwema, alisema: "Sampuli zitakazochukuliwa kutoka kwa majeruhi wa ajali hiyo ili kuwatambua ni kutoka kwa wazazi, watoto na ndugu wa karibu wa majeruhi hao."

Ajali hiyo ilitokea Jumamosi asubuhi eneo la Msamvu mkoani Morogoro baada ya lori lililokuwa limebeba tangi la mafuta ya petroli, kuanguka na baadaye kulipuka wakati baadhi ya wananchi wakichota mafuta yaliyokuwa yanamwagika kutoka kwenye tangi hilo.

DEREVA ALIYEKIMBIA

LORI RUVUMA MBARONI

Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia Hubert Mpete (51), mkazi wa Njombe ambaye pia ni dereva wa gari lililokuwa limesheheni petroli likitokea mkoani Njombe kwenda Songea ambalo liliacha njia kisha kugonga mti na kuwaka moto.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Jumapili saa nne usiku katika Kijiji cha Hanga Ngandinda wilayani Songea.

Alisema gari lenye namba za usajili T 243 DCU na tera mali ya mfanyabiashara James Mwinuka, mkazi wa Njombe ambaye pia ni mmiliki wa kituo cha mafuta cha Njombe Filling Station.

Alisema siku ya tukio, Mpete alikuwa akiendesha gari hilo kwa mwendokasi, hivyo kumshinda, kuacha njia kisha kuelekea porini na kugonga mti kulikosababisha kichwa cha gari kuwaka moto na kuteketea.

Alisema baada ya kupata taarifa ya ajali hiyo, Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji walifika katika eneo hilo na kukuta gari likiwaka moto na kufanikiwa kuokoa mafuta yenye ujazo wa lita 33,000 na kuuzima moto huo kabla ya kutokea madhara.

Kamanda Maigwa alisema dereva huyo amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma akiendelea kupatiwa matibabu chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi na hali yake ya kiafya ikitengamaa, utaratibu wa kumhoji utaendelea ili baadaye afikishwe mahakamani.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Magafu Majura, alithibitisha kuwapo kwa majeruhi huyo katika hospitali yake, akieleza kuwa anasumbuliwa na maumivu ya kifua na paja la mguu wa kulia.

Habari Kubwa