Ndalichako aagiza watafiti kutengeneza teknolojia rahisi

15Aug 2019
Allan lsack
ARUSHA
Nipashe
Ndalichako aagiza watafiti kutengeneza teknolojia rahisi

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, ameviagiza vituo na taasisi za utafiti kutengeneza teknolojia rahisi, itakayorahisisha na kuchochea maendeleo kwa wananchi.

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa tatu wa kimataifa wa nishati endelevu na technolojia ya maji katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela(NM-AIST), Ndalichako alisema ni wakati kwa vituo vya utafiti na taasisi zinazojihusisha na tafiti, kubuni teknolojia rahisi itakayochangia kuchochea maendeleo kwa kasi katika jamii.

Alisema kuwa sayansi na teknolojia ni nyenzo muhimu ya kuleta maendeleo ya kiuchumi, endepo kutatumika teknolojia rahisi ambayo itawawezesha wananchi wengi hususan maeneo ya vijijini kupata maendeleo kwa wakati.

Hata hivyo, alisema serikali imejenga mifumo na miundombinu pamoja na kutenga bajeti kubwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo wananchi, kufahamu umuhimu wa utafiti unaofanywa na watafiti nchini.

Alisema sera ya serikali ya mwaka 2015/2025, ni kufikia uchumi wa viwanda na sera hiyo, inaendana na sera ya kimataifa ya maendeleo endelevu.

“Mwaka 2017, nilikuja hapa Nelson Mandela, kuzindua vituo vinne vya umahiri vya sayansi na teknolojia vya elimu ya juu, ambavyo vilianzishwa na serikali kupitia mkopo nafuu kutoka benki ya dunia kwa lengo la kuboresha utafiti ambao utaleta matokeo chanya kwa wananchi,” alisema Ndalichako na kuongeza: “Furaha yangu baada ya miaka miwili kupita vituo vinne nilivyovizindua vimeanza kazi ya kuboresha utafiti na kuleta matunda ya nchi.”

Alisema lengo la serikali kufikia uchumi wa viwanda, hivyo watatoa elimu na kuendeleza ujuzi kwa wananchi, ili wawe na uwezo wa kuongeza thamani ya bidhaa wanazozalisha kwa kutumia teknolojia rahisi na ya kisasa.

Dk. Yusufu Jande, Kiongozi Msaidizi kutoka Kituo cha Umahiri cha Miundombinu ya Maji na Nishati Endelevu cha Wise- Future, alisema nchi 11, zimeshiriki katika mkutano huo wa kimataifa ni Korea Kusini, Nigeria, Namibia, Indonesia, Ufaransa, Uingereza, Tanzania, Kenya na Uganda.Alisema lengo la kuwakutanisha watafiti kutoka nchi hizo ni kujadiliana namna ya kuvumbua mambo kupitia kazi za utafiti wanaofanya.

Aidha, alisema kuwa kupitia utafiti wanaofanya wamegundua teknolojia rahisi ya kuondoa madini ya floride, vijidudu na chumvi chumvi katika maji.Alieleza kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanyika awali, kiasi cha chumvi katika maji kinatakiwa kuwa miligramu 500, kwa lita moja ya maji.

Mkuu wa Chuo cha Nelson Mandela, Prof. Emmanuel Luoga, alisema chuo hicho, kimejikita zaidi katika utafiti wa nishati endelevu ya jua na maji kwa kushirikiana na nchi washiriki wa mkutano pamoja na vituo vya utafiti vya iTEC.

Habari Kubwa