Mhadhiri NIT kortini madai ya kuomba rushwa ya ngono

15Aug 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mhadhiri NIT kortini madai ya kuomba rushwa ya ngono

MHADHIRI wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Samson Mahimbo (68), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na tuhuma za kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wa chuo hicho.

Mhadhiri huyo ambaye alikuwa akifundisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza 2015/16, anadaiwa kuomba rushwa hiyo kutoka kwa mwanafunzi Victoria Faustine.

Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Vera Ndeoya, alidai kuwa Januari 12, 2017 katika nyumba ya kulala wageni, iliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam, mshtakiwa aliomba rushwa ya ngono.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo akiwa mwajiriwa wa NIT katika kozi ya Usimamizi wa Barabara na Usafirishaji namba LTU 07101 kwa kutumia mamlaka yake, alimlazimisha mwanafunzi huyo kutoa rushwa ya ngono.

Ilidaiwa kuwa aliomba rushwa hiyo ili aweze kumfaulisha katika mtihani wake wa marudio katika kozi ya Usimamizi wa Barabara na Usafirishaji anayosomea ya Januari 5, 2017.

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo.

 

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba tarehe ya kuanza kusikilizwa.

Hakimu alimtaka mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini hati ya dhamana ya Sh. milioni nne na alitimiza masharti hayo.

Alisema kwa kuwa mshtakiwa ametimiza masharti ya dhamana atakuwa nje mpaka Septemba 17, mwaka huu, kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa.

Habari Kubwa