Shahidi akana mawasiliano na Zitto

15Aug 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Shahidi akana mawasiliano na Zitto

Uvinza, Petro Salum (50), amedai mahakamani kwamba hajawahi kuwasiliana na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, kuhusu idadi ya watu waliokufa katika operesheni ya kuwaondoa wananchi waliokuwa wakiishi maeneo ya hifadhi ya wanyama Uvinza.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe

MWENYEKITI wa Kijiji cha Mpeta

Salum ambaye ni shahidi wa Jamhuri katika kesi ya uchochezi inayomkabili Zitto, alitoa ushahidi wake jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, shahidi alidai Mkuu wa Wilaya ya Uvinza alimfahamisha kwamba wananchi wanatakiwa kuhamishwa katika hifadhi hiyo, hivyo alikuwa akiomba eneo la kuwahamishia.

Shahidi alidai alikaa na halmashauri ya kijiji, eneo lilipatikana hivyo wananchi waliwapa elimu kutoka katika eneo la hifadhi.

Alidai kuwa baada ya kupatikana eneo, operesheni ya kuwahamisha ilianza kwa kuwatumia askari wa wilaya, mgambo na wananchi na Oktoba 15, 2018 alipata taarifa kuna vurugu ilitokea.

Alidai kuwa alikwenda kuonana na diwani; “lakini hatukuweza kuzuia tukabakia tumekaa hadi Oktoba 18, 2018 nilipopigiwa simu na Mkuu wa Wilaya niende, nilipofika niliwakuta Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa, wakasema walishindana na wananchi wanaomba msaada tuende porini kutafuta miili ya marehemu.”

"Mheshimiwa hakimu tulikwenda porini Oktoba 19, 2018 tukafanikiwa kupata miili ya marehemu wawili askari na baadaye ilifahamika kuna raia wengine wawili walifariki katika operesheni hiyo na kufanya idadi ya waliokufa kufikia wanne," alidai shahidi huyo.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Mkuu wa Kituo cha Polisi na polisi anayeitwa Muddy na kwa upande wa raia walikufa wawili.

Shahidi alidai, jina la Zitto analisikia, lakini hajawahi kuwasiliana naye kuhusu idadi ya waliokufa katika operesheni hiyo.

Katika kesi ya msingi, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi. Anadaiwa kutenda makosa hayo, Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT-Wazalendo.

Habari Kubwa