Lissu, Ndugai kuwasha moto mahakamani leo

15Aug 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Lissu, Ndugai kuwasha moto mahakamani leo

MAOMBI ya kesi namba 18 ya mwaka 2019 yaliyofunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kupitia kwa mawakili wake dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, yanatarajiwa kuanza kusikilizwa leo katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dar es Salaam.

Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu

Katika kesi hiyo, Lissu anapinga uamuzi wa Spika Ndugai wa Juni 28, mwaka huu wa kumvua ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chadema, Tumaini Makene, ilieleza kuwa maombi hayo yatasikilizwa mbele ya Jaji Mtupa.

Katika taarifa yake hiyo, Makene alisema hati ya wito wa mahakama inabainisha kuwa mlalamikiwa ambaye ni Spika Ndugai, atatakiwa kufika mahakamani bila kukosa akiwa na nyaraka zote anazotakiwa kuwa nazo kwenye shauri hilo.

"Tunatoa wito kwa viongozi, wanachama, wafuasi wa Chadema na Watanzania wote wapenda haki, demokrasia na utawala bora unaoheshimu sheria, mahali popote walipo kufuatilia kwa karibu mwenendo wa shauri hilo kuanzia hatua ya sasa na kipekee kupata muda wa kufika mahakamani kuungana pamoja na kusikiliza mapambano hayo ya kuitafuta haki ya Tundu Lissu," Makene alieleza katika taarifa yake hiyo.

Alisema wameamua kutafuta haki mahakamani baada ya Spika Ndugai kutangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu Juni 28, mwaka huu, alipokuwa akiahirisha mkutano wa Bunge la Bajeti jijini Dodoma.

Lissu ambaye pia alikuwa Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, yuko Ubelgiji akiendelea na matibabu ya kibingwa baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana wakati akijiandaa kushuka kwenye gari lake nyumbani kwake mjini Dodoma Septemba 7, 2017.

Baada ya kunusurika kifo katika shambulio hilo, Lissu alipatiwa matibabu ya awali katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma na baadaye kusafirishwa kwenda Hospitali ya Nairobi, Kenya kwa matitabu ya dharura kisha kuhamishiwa Ubelgiji ambako amekuwa akipata matibabu tangu Januari 2018.

Mwanzoni mwa mwaka huu, afya ya Lissu ilionekana kuimarika alipofanya ziara katika nchi kadhaa za Ulaya na Amerika na kuzungumza na vyombo vikubwa vya habari, akiilaumu Serikali ya Tanzania kwa kushindwa kuwapata waliomshambulia.

Mtalaamu huyo wa sheria  pia aliweka wazi kuwa atawania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao ikiwa chama chake kitaamua hivyo huku akitangaza kuwa amepanga kurejea nchini Septemba 7, mwaka huu, tarehe aliyoshambuliwa mwaka juzi.

Habari Kubwa