Wananchi waambiwa wanywe chai kujitibu

16Aug 2019
Jaliwason Jasson
MANYARA
Nipashe
Wananchi waambiwa wanywe chai kujitibu

MTAALAMU wa masuala ya lishe amewashauri wakulima kuzalisha chai kwa wingi kwa vile ina faida lukuki ikiwamo kutibu magonjwa mbalimbali.

Aidha, chai inatajwa kuwa inasaidia kuimarisha viungo vya mwili na pia ni dawa inayomwepusha mtumiaji na maradhi, hivyo kuepuka gharama za matibabu.

Ushauri huo ulitolewa jana na mtaalamu wa lishe wa Shirika la Taha, Rozalia Aloyce, alipozungumza na Nipashe juu ya faida za chai.

"Chai inasaidia kuimarisha mifupa na kupambana na magonjwa ya sukari na magonjwa mengine mengi," alisema Aloyce.

Alieleza kuwa zao hilo si geni nchini na kuongeza kuwa  mbegu zake zimeanza kuingia kutoka  Kenya na kwamba linafaa kwa  biashara, hivyo wakulima waanze kulichangamkia.

Alisema mtu akitumia chai kama alikuwa ameanza kuchoka na kuzeeka usoni, inamsaidia kubadilisha mwili wake na kuonekana  kijana japo  umri ni mkubwa.

Baadhi ya wakazi wa Babati, akiwamo  Keneth Daud alisema ni mara ya kwanza kulisikia kama lina faida za kutibu maradhi, hivyo aliishauri serikali kulihamasisha lilimwe na matumizi yake yahamasishwe, ili watu waweze kupata tiba na kuepuka kemikali za dawa za kisasa.

Kwa upande wake Kemilembe Novath, mkazi wa Kagera anayeishi Babati kimatembezi alisema, zao hilo  linalimwa sana Wilaya ya Karagwe, hivyo wenye uhitaji wanaweza kupata mbegu huko bila shida.

Alisema wakulima wengi mkoani Kagera wanalichangamkia kulilima, ila changamoto iliyopo ni ya wanunuzi ambao ni wachache.

Chai inaelezwa kuwa inatibu ugonjwa wa sukari, hivyo ni vyema wataalamu wa kilimo wakalipa kipaumbele na wataalamu wa afya waendelee kulifanyia utafiti kama linatibu sukari na kung'arisha miili ya watu.

Habari Kubwa