Wadau wa lishe washiriki kukabiliana na udumavu

16Aug 2019
Woinde Shizza
ARUSHA
Nipashe
Wadau wa lishe washiriki kukabiliana na udumavu

WADAU wa masuala ya kuboresha lishe wakiwamo wazalishaji na wasindikaji wanaoongeza thamani bidhaa za chakula, wametakiwa kutokomeza udumavu kwa kuwa unawaumiza zaidi watoto wengi huko vijijini.

Mratibu wa Asasi ya Infoy inayoshughulika na masuala ya chakula, Laurent Sabuni, alisema hayo jana katika maonyesho ya bidhaa za lishe, yaliyoandaliwa na shirika hilo kwa kushirikiana na shirika la kuhudumia viwanda vidogo (Sido) mkoa wa Arusha.

Alisema wazalishaji na wasindikaji wa bidhaa za lishe, wanapaswa kushiriki kutatua matatizo ya lishe duni katika jamii na kuhakikisha kuwa wanazifikisha bidhaa hizo vijijini.

Sabuni alisema kuwa wamekuwa wakitoa mafunzo kwa wasindikaji wa bidhaa za lishe juu ya namna bora ya kusindika na kuzifungasha, ili ziweze kuwafikia wateja na kusaidia kupunguza tatizo la udumavu, linalowakabili watoto wengi nchini.

Meneja wa Sido Mkoa wa Arusha, Nina Nchimbi, aliwataka wasindikaji na watengeneza unga wenye virutubisho na viini lishe, ili kukidhi afya ya mlaji na kuhakikisha suala la viwango vya ubora katika bidhaa za lishe wanazozalisha unazingatiwa.

Nina alisema kuwa Sido imefanya juhudi za kuwaunganisha wajasiriamali hao na taasisi za kudhibiti ubora ikiwamo TBS ili bidhaa zao zithibitishwe ubora na kupata masoko ya kitaifa na kimataifa.

Kwa upande wao wasindikaji na wajasiriamali wa bidhaa za lishe, Dorice Assenga na Walter David walisema wamekuwa wakitoa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya unga wa lishe kwa watoto wadogo na kuzipeleka bidhaa hizo maeneo ya pembezeni, ambako kuna hitaji kubwa la lishe, ili kuwasaidia kinamama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Mtaalamu wa Lishe, Prisca Mwakalasi, alisema kuwa mchango wa wadau wa lishe ni mkubwa, kwani madhara ya udumavu huonekana hasa mtoto anapokuwa na kuwa mtu mzima na inakuwa vigumu kufanya maamuzi sahihi.

Alieleza kuwa ni kwa sababu anakua amedumaa hadi akili, hivyo masuala ya lishe kwa watoto na watu wazima yanapaswa yapewe kipaumbele kwani lishe ni kiini cha maendeleo.