Wafanyakazi watinga  kwa DC kuhoji hatima

16Aug 2019
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Wafanyakazi watinga  kwa DC kuhoji hatima

WAFANYAKAZI zaidi ya 300 wa kampuni ya ulinzi tawi la Arusha, wametinga Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Arusha Gabriel Daqarro, kutoa malalamiko na kuhoji hatima ya mafao yao.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Gabriel Daqarro

Watumishi hao kutoka kampuni ya Ultimate Security wanalalamikia kuuzwa kinyemela kwa kampuni hiyo, bila wao kushirikishwa na hawafahamu hatima ya stahiki zao.

Wakiongea na vyombo vya habari baada ya kupeleka malalamiko yao kwa mkuu huyo, kwa niaba ya wenzao, Abedy Ally, Baraka Makala na Alex Mollel, wamelalamikia kampuni hiyo kuuzwa bila kuelezwa mustakabali wa stahiki zao licha ya kufanyakazi kwa muda mrefu.

Walisema kuwa kampuni ya Ultimate imeuzwa kwa kampuni mpya Gardaworld, jambo ambalo wanahofu kupoteza stahiki zao baada ya mabadiliko hayo, huku wakimtaka mmiliki mpya wa kampuni ya Gardaworld kujitokeza ili kuwahakikishia stahiki zao.

"Sisi tutapataje haki zetu na tumefanya kazi  miaka mingi, katika kampuni hii, tunaomba Mkuu wa Wilaya utusaidie katika hili, maana hata hatujashirikishwa katika maamuzi haya," alisema Alex Mollel.

Akiongelea suala hilo Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro, alisema mabadiliko ya umiliki wa kampuni ya Ultimate kwenda kwa kampuni ya Gardaworld yapo kisheria, isipokuwa aliutaka uongozi wa Ultimate kukaa na wafanyakazi hao na kuwaelimisha mabadiliko hayo.

"Msihofu ondoeni hofu wala hawajauza kinyemela kila kitu katika mauzo haya kati ya kampuni hizi yapo kisheria ila nawaomba nyie uongozi wa Ultimate kaeni na wafanyakazi wenu waelezeni mabadaliko haya ili kuondoa sintofahamu inayojitokeza kwao," alisema.

Kwa upande wake, Eliuta Mjawike, ambaye ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ulinzi ya Ultimate Tanzania, aliwahakikishia wafanyakazi hao kuwa hawatapoteza haki zao baada ya kutokea mabadiliko ya umiliki wa kampuni hiyo.

Alisema hakuna haja ya kupata hofu sababu wafanyakazi hawajauzwa kama wanavyodai, ila mabadiliko hayo yametokana na kampuni ya Ultimate kuuzwa hisa zake asilimia 100 kwa kampuni hiyo ya Gardaworld ya nchini Canada na hivyo wafanyakazi hawataathirika popote na mabadiliko hayo.

"Mfanyakazi yeyote wa Ultimate hatapoteza stahiki zake kwa haya mabadiliko yaliyofanyika kutoka kampuni ya ultimate kwenda kuwa Gardaworld kwa sababu mikataba yao ipo kisheria na wasiwe na hofu," alisema Mjawike

Meneja wa Ultimate Kanda ya Arusha na Moshi, Abdallah Ally, alisema kuwa kampuni hiyo ina jumla ya wafanyakazi 325 katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro na changamoto iliyojitokeza ya wafanyakazi kwenda ofisi za Mkuu wa Wilaya, ni kutokana na baadhi yao kutopata elimu juu ya mabadiliko yaliyojitokeza.

Kampuni ya Gardaworld yenye makao yake nchini Canada inaelezwa pia kuwa imenunua kampuni nyingine mbili za ulinzi  na kwamba  zitaunganishwa kabla ya kuanza majukumu.