Agizo la Jafo lapokewa kwa mitazamo tofauti

16Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
SAME
Nipashe
Agizo la Jafo lapokewa kwa mitazamo tofauti

WATU wa kada mbalimbali wilayani hapa wamelipokea kwa hisia tofauti agizo la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, kutaka wakurugenzi wajieleze.

Juzi, Jafo aliwataka wakurugenzi wa halmashauri za wilaya ambazo zimefanya vibaya kwenye utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo, kujitathmini na kuandika barua ya kujieleza ndani ya siku 14.

Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro ni miongoni mwa halmashauri zilizotajwa na  Jafo kwamba ziko kikaangoni kutokana na kufanya vibaya katika utoaji wa fedha hizo.

Mwanasiasa na mkazi wa Hedaru, Wilaya ya Same, Christopher Mbajo, alisema kwa halmashauri hiyo kuingia katika kundi hilo, ni tatizo ambalo linatokana na ama mfumo wa siasa kutishiwa na itikadi za kisiasa au uongozi kushindwa kusimamia makusanyo ya fedha na mgawanyo wake.

"Kama kweli tunataka kuendeleza jitihada za kupambana na umaskini hasa katika maeneo ya vijijini na kuongeza fursa za ajira ili kuharakisha maendeleo, serikali inapaswa kuchunguza kwa makini ni kipi kisababishi chake hadi halmashauri yetu kushindwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo. Isiishie kwa ma DED (Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya) tu kuandika barua za kujieleza," alisema Mbajo.

Halmashauri ya Wilaya ya Same iliyoanzishwa rasmi kwa Sheria ya Bunge, Sura ya 287 (Mamlaka za Wilaya) ya Sheria za Tanzania na kuanza kutekeleza majukumu yake Januari Mosi, 1984, imetajwa kuchangia asilimia nne.

Mchungaji wa Usharika wa Makasa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Pare, Elisa Mrutu, alisema tatizo si wakurugenzi bali ni mfumo mpya wa ukusanyaji wa mapato yanayopatikana na upelekaji wa pesa hizo zinazokusanywa katika mfuko mkuu wa serikali.

"Nasema hivyo kwa sababu kuna kitu kinaitwa OC (fedha za matumizi mengineyo) ambazo haziji kwa wakati katika halmashauri na zikija zinakuja chini ya asilimia 50. Unategemea mkurugenzi labda alitaka kutekeleza kipaumbele cha kujenga madarasa au vituo vya afya, fedha atatoa wapi?

"Mfumo huo mpya unaleta changamoto hasa unapopeleka fedha kwenye mfuko mkuu wa hazina na zile pesa walizokuwa wanategemea wanakosa na halmashauri sasa hivi ziko hoi. Walete hela kwa wakati waone kama hazitachangia katika miradi ya maendeleo," alisema.

Naye Furaha Mgonja, mkazi wa kata ya Stesheni, alitaka kujua sababu gani za msingi zinazoifanya serikali kutowabana mapema watendaji hao wa halmashauri na kuwaacha hadi kushindwa kufikia lengo lililowekwa.

Aidha, katika taarifa hiyo ya Waziri Jafo, alinukuliwa akisema wakurugenzi 102 wameshindwa kuchangia katika miradi ya maendeeo kwa asilimia 20.

Habari Kubwa