Barabara kujengwa kwenda Ziwa Ngozi

16Aug 2019
Grace Mwakalinga
MBEYA
Nipashe
Barabara kujengwa kwenda Ziwa Ngozi

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Kanda ya Mbeya, umeahidi kuboresha miundombinu ya barabara kwenda kwenye kivutio cha utalii cha Ziwa Ngozi ili kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi.

Meneja wa TFS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Ebrantino Mgiye, alisema  hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kivutio hicho.

Mgiye alisema wako kwenye mchakato wa kukusanya fedha kwa kushirikiana na wadau wengine wa utalii ili kutengeneza miundombinu ya barabara kuelekea kwenye kivutio  cha Ziwa Ngozi.

"Hivi karibuni Ziwa Ngozi limekuwa kivutio kutokana na mwonekano wake mithili ya ramani ya Afrika, njia zinazotumika kufikia ziwa hilo ni za kuvutia na kusisimua kwani zimejaa milima na miteremko, hali ya hewa lakini pia maji yaliyopo ndani ya ziwa hilo kitu ambacho kimesababisha kuvutia watalii wengi,” alisema Mgiye.

Mgiye alisema Ziwa Ngozi kuwa na miundombinu ya kuridhisha hasa barabara litawezesha watalii wanatembelea kivutio hicho kwa lengo la kujionea uzuri na maajabu yake.

Ziwa Ngozi ambalo liko katika safu za Milima ya Uporoto inayopakana na Wilaya za Mbeya na Rungwe lina urefu wake wa kilometa 2.5, upana kilometa 1.6 kina chake kwenda chini ni mita 74. Ziwa hilo ni pili kwa ukubwa katika maziwa yatokanayo na kreta barani Afrika.

Mdau wa utalii mkoani Mbeya, Amos Mwamugobole, alisema Ziwa Ngozi ni miongoni mwa vivutio vinavyopendwa na watalii kutokana na upekee wake ambao huwavutia.

Alisema kutokana na fursa zilizopo ndani ya ziwa hilo, wadau wa utalii akiwamo  yeye, huandaa matembezi ya mara kwa mara kutembelea kivutio hicho.