Pinda ampamba JPM utendaji safi

16Aug 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Pinda ampamba JPM utendaji safi

WAZIRI Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, ameipongeza serikali kwa kazi kubwa na ya kipekee kwenye miradi ya maendeleo, hususani sekta ya afya, maji, miundombinu na umeme.

WAZIRI Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda na Rais John Magufuli

Akizungumza wakati wa kupokea Mwenge wa Uhuru jijini Dodoma, uliopokelewa Nzinje  katika kata ya Zuzu, Pinda alisema kuna kila sababu ya kumpongeza Rais John Magufuli kwa sababu utendaji wake ni wa kipekee.

Alisema  amekuwa jasiri wa kuamua kufanya maendeleo bila kuhofia kitu chochote kitendo kinachomtofautisha na utendaji wa awamu nyingine.

Alisema mradi wa uzalishaji umeme (stiegler's Gorge) awali ilidaiwa utasababisha uharibifu wa mazingira kitu ambacho Rais Magufuli amethubutu kukipuuza na kuanza kutekeleza mradi.

"Kwa kweli Rais Magufuli anastahili pongezi katika ujenzi wa miundombinu kwa ujumla hata wale wanaopinga baadhi ya mambo wanapaswa kumpongeza," alisema Pinda.

Kuhusu ununuzi wa ndege, alisema awali katika mitandao ya kijamii baadhi ya watu walionekana wakimlaumu ya kuwa zinalitia hasara taifa ili hali kipindi kile ilikuwa ni majaribio.

Alisema hivi sasa ndege hizo zinafanya safari mara mbili kwa siku na abiria wanapanda kwa wingi jambo ambalo linaingiza faida kubwa ikiwamo kuchangia kuongeza uchumi wa nchi kupitia mapato yanayopatikana.

"Tujifunze kuweka akiba ya maneno natamani hivi sasa niwaulize, waliokuwa wakitoa lawama hizo, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni," alisema Pinda.

Aliongeza kuwa kwenye miundombinu ya barabara serikali imeipa kipaumbele kutokana na kwamba barabara nyingi zimeboreshwa jijini Dodoma na maeneo mengine jambo ambalo limesaidia kurahisisha utendaji kazi wa wananchi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Awali, akisoma taarifa ya mradi wa ufugaji samaki wa Pinda Farm, mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Tunu Pinda alisema ufugaji samaki shambani kwao Pinda Products Farm, alisema  ni miongoni mwa miradi michache ya ufugaji samaki iliopo jijini hapa.

Alisema mradi huo umegharimu Sh. milioni 29 kujenga mabwawa saba, yakiwamo madogo sita na kubwa moja ambayo yanazalisha sato na kambale.

Alisema changamoto zinazowakabili katika mradi huo ni pamoja na upatikanaji wa chakula cha samaki cha uhakika kwa bei nafuu hapa nchini, ambapo chakula hicho kinatengenezwa nje ya nchi ikiwamo kuuzwa kwa gharama kubwa ikichangiwa na usafirishaji.

Alisema kutokana na hilo wananchi wa kata ya Zuzu wameiomba serikali isaidie wafugaji wa samaki kupata elimu ya kutosha kuhusu uwekezaji huo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, vijana Ajira, Anthony Mavunde, alimpongeza Pinda kwa kazi nzuri ya ufugaji anayofanya na kwamba amesaidia kuongeza ajira kwa vijana wa eneo hilo.

"Nakupongeza sana mstaafu kwa kusaidia kuongeza ajira kwa vijana nami kama mbunge na waziri nitaendelea kuhimiza upatikanaji wa Umeme Vijijini -Rea," alisema Mavunde.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Mzee Mkongea Ally, alisema mradi huo ni darasa kwa wakazi wa eneo hilo na jamii kwa ujumla kwa sababu wengi wanapita kujifunza kupitia shamba hilo.

Habari Kubwa