Wakumbushwa fursa za zabibu SADC

16Aug 2019
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Wakumbushwa fursa za zabibu SADC

WAKULIMA wa zabibu na wasindika mvinyo wametakiwa kutumia fursa ya Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kujipatia soko la uhakika la  bidhaa hiyo.

zabibu

Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, wenye viwanda na kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Dodoma, Idd Senge, alisema wakati alipokuwa akizungumza na wanahabari.

Alikuwa akizindua jukwaa la wadau wa zabibu jijini Dodoma.

Tanzania inazalisha zabibu kwa wingi katika jumuiya ya  SADC hivyo, ni fursa kwa wakulima pamoja na wasindikaji wa mvinyo kujipatia soko la uhakika la zao hilo.

Senge, alisema zipo nchi nyingi katika jumuiya hiyo ambazo hazilimi kabisa zabibu hivyo wakulima wakichangamkia fursa hiyo kwa kutafuta masoko katika nchi hizo watakuwa wametibu shida ya ukosefu wa soko.

"Katika jumuiya hii nchi ambayo inalima kwa wingi ikiondoa Tanzania ni Afrika Kusini, lakini zipo nyingine ambazo hazilimi kabisa hivyo sisi tutatumia fursa hii kupata soko kuuza mvinyo au kusafirisha juisi ya  zabibu," alisema Senge.

"Hivi sasa zabibu nyingi zinaozea mashambani kutokana na kukosa soko kwa vile wazalishaji ni wachache, hivyo kuelemewa na kile wanachozalisha wakulima," alisema Senge.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobas Katambi, akizungumza wakati wa uzinduzi wa jukwaa hilo la wadau wa zabibu alisema kuwa vijana wanatakiwa kubadili mitazamo yao na kuingia katika kilimo cha zabibu ambacho kitaweza kuwakwamua kiuchumi.

"Katika mataifa makubwa kama Marekani wakulima ndiyo watu wenye fedha kuliko makundi mengine, lakini huku kwetu vijana wanaona kilimo kama kazi ya wazee, hali ambayo siyo kweli kwani kilimo kinaweza kuwatoa vijana kuliko kitu kingine," alisema.

"Kama kijana ataingia katika kilimo cha zabibu basi kinaweza kumkomboa kwa sababu zabibu ukilima leo unavuna mfululizo ndani ya miaka zaidi ya 60, hivyo hata watoto wako hadi wajukuu wanaweza kufaidika nayo harafu sasa kwa neema za mungu hapa kwetu tunavuna mara mbili kwa mwaka tofauti na maeneo mengine duniani," alisema Katambi.

 Mkurugenzi wa Baraza la Kilimo, Timoth Mbaga, alisema lengo la kuanzisha jukwaa hilo ni kusaidia kuinua zao hilo la zabibu ambalo kama litasimamiwa linaweza kuitangaza Tanzania kimataifa.