Waziri apigia debe utalii wa majahazi

16Aug 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Waziri apigia debe utalii wa majahazi

WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo, amesema utalii wa majahazi ni kivutio kikubwa cha watalii licha ya kwamba Zanzibar inapokea watalii wengi wanaosafiri kwa kutumia ndege.

majahazi

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza katika hafla ya kumuaga Nassir Salum Mabrouk ambaye atashiriki tamasha la safari ndefu duniani kwa kutumia usafiri wa boti katika kutembea dunia nzima kupitia baharini.

Alimtaka mshiriki huyo ambaye ni pekee kwa nchi za Afrika Mashariki kuitangaza Zanzibar kiutalii kupitia mashindano hayo.

Kombo alisema iko haja sasa ya kukuza utalii wa bahari ili watalii wanaofika Zanzibar watumie usafiri wa baharini.

"Nikupongeze sana kwa ujasiri wako maana huko unakwenda katika safari ndefu ambayo utatumia boti ambayo haina mashine," alisema waziri huyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Nassir alisema anatumaini atarudi na ushindi mzuri na ataitangaza Zanzibar kimataifa kupitia mashindano hayo.

Alisema mashindano hayo ya tamasha la safari ndefu duniani, anatumia boti ambayo haitumii mashine na badala yake itakua inategemea upepo na watazunguka mabara sita.

"Tunategemea kuanza safari Septemba, mwaka huu na kumalizia Agosti, mwakani  na tutaanzia London (Uingereza), Ureno, Uruguay, Cape Town (Afrika Kusini), Australia, China, New York (Marekani), Bermuda, Ireland na kurejea London," alisema.

Aidha, alisema nchi 11 zitashiriki katika tamasha hilo na kwa Afrika Mashariki yeye ni mshiriki pekee.

Nassir alisema ana uzoefu wa kutembea na majahazi masafa marefu na amekuwa akitoka Unguja hadi Pemba kwa kutumia usafiri wa jahazi akiwa baharini na kwamba jahazi hilo linategemea upepo pekee.

"Sijawahi kusafiri kwenda Pemba kwa kutumia boti au ndege. Naondoka kwa kutumia jahazi ambalo linatumia upepo pia nimeshasafiri kwa kutumia jahazi kutoka Zanzibar hadi Madagascar tena nakwenda na kurudi salama," alisema.

Alisema usafiri wa baharini ni mzuri licha ya kwamba una changomoto nyingi lakini unamjengea ujasiri na ustahamilivu.

Hata hivyo, alisema changamoto kubwa iliyopo katika usafiri wa majahazi ni pale linapokatika tanga na kupoteza mwelekeo wa safari na upepo hukupeleka popote hivyo inabidi uvumilivu.