Mradi unaowanasua waliokwama baada ya shule hadi ujasiriamali

16Aug 2019
Yasmine Protace
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mradi unaowanasua waliokwama baada ya shule hadi ujasiriamali

YANAPOZUNGUMZIWA makundi, zaidi inamaanisha mkusanyiko wa watu kwa ajili ya kutekeleza nia fulani ya kijamii. Ni kawaida, makundi yanakuwa kwa maana maalum na matunda ya kazi zake kusifiwa kuwa chanya zaidi.

Wanakikundi wakijifunza ujasiriamali katika Kata ya Ukonga.

Hata itakumbukwa kaulimbiu iliyotumika zaidi nchini na hasa baada ya uhuru “Umoja ni Nguvu, Utengano ni Udhaifu” ilibeba ujumbe mkubwa kuonyesha inatoa matunda chanya katika kila kinachotekelezwa katika mfumo wa kujumuika.

Kuna makundi yanaanzishwa kwa ajili ya kufanya mradi au kufanya jambo fulani, ikinuia kwa ajili ya maendeleo mbayo yanashuka hadi ngazi ya maisha ya mtu mmoja mmoja.

Serikali kupitia njia hiyo imekuwa ikihamasisha vijana wajiunge katika makundi ili waweze kunufaika na mikopo ambayo imekuwa ikitolewa na Serikali kwa ajili ya ujasiriamali.

Hata benki nyingi na asasi nyinginezo za kifedha, zimekuwa na kanuni, miongozo na sheria, zinazowezesha watu kupata mikopo katika njia ya vikundi.

Jumuiya za ushirika wa aina mbalimbali, ikiwamo ya kuweka na kukopa maarufu kama ‘saccos’ nazo ni mazingira ambayo yanawawezesha watu kukopeshana ndani ya mjumuiko wa kijamii.       

Katika hilo, mikopo inayotolewa na Serikali kwa vijana imekuwa mkombozi kwao kuwainua kimaendeleo na hasa kiuchumi.

Naibu Meya

Naibu Meya Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam, Omary Kumbiramoto, anawataka vijana wachangamkie mikopo kwa nia ya kunufaika nayo

Ni kauli aliyoitoa alipofungua mafunzo ya mwezi mmoja kwa watoto waliotoka katika mazingira magumu, katika Kata ya Ukonga.

" Nawapongeza viongozi wa Kituo cha Maarifa Kipunguni, kwa kuwakumbuka watoto walio na mazingira magumu na kuamua kuwapatia elimu bure, ili waweze kujiongezea kipato," anasema. 

Naibu Meya anafafanua kwamba Serikali inayasaidia makundi maalumu, kwa kutatua changamoto zao, ikiwamo kuwawezeshea mikopo wanawake na vijana.

Anawaasa vijana kwamba ni jukumu lao kujiunga katika makundi, ili wanufaike kiuchumi kupitia daraja la mikopo na akiwakumbusha kwamba elimu inayotolewa na kituo itawasaidia vijana hao kujiongezea kipato. 

Mkurugenzi

 Mkurugenzi wa Kituo cha Maarifa ya Jamii, Selemani Bishagazi, anasema jumla ya vijana 100 watanufaika na mafunzo hayo, kutoka kwa walimu wataalamu waliobobea katika stadi ya ujasiriamali.

"Mafunzo haya ni ya mwezi mmoja, yanatolewa na hakuna gharama zozote ambazo watalipa. Watajifunza kutengeneza mifuko, mishumaa, batiki, kuweka dawa, kichwani, kutengeneza keki, kupamba ukumbi na kilimo cha mbogamboga," anaeleza.

Bishagazi anasema kuwa mafunzo hayo yanatolewa katika Kata ya Ukonga, ambako vijana wanaoishi katika mazingira magumu kutoka maeneo mbalimbali ya kata watanufaika na mafunzo hayo.

Mwenyekiti wa Sauti ya Jamii, Fatma Abdulrahman, anasema wamekuwa wakiiangalia jamii inayowazunguka na kubaini watoto wengi hawajaendelea au kupiga hatua ndogo, baada ya kumaliza elimu za msingi na sekondari.

Anasema baada ya kubaini hilo, waliamua kuwachukuwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kuwafundisha elimu ya ujasiriamali, ili iweze kuwa mkombozi katika maisha yao.

Anasema mafunzo hayo pia yalishatolewa kwa wasichana 30 manusura wa kukeketwa. Fatma anafafanua: "Wasichana walionusulika kukeketwa walifundishwa kupambana, kilimo na ufundi wa kushona nguo."

Wito wa Fatma ni kwamba, wazazi na watoto wanaoishi katika mazingira magumu wajitokeze kupatiwe elimu itakayokuwa mkombozi kwao.

Mkurugenzi wa kampuni ya CSI, Upendo Invocaviti, ambao ndio walifadhili mafunzo hayo, anaeleza historia yao kwamba kampuni ilianzishwa mwaka 2011, lengo ni kuleta usawa kwa jamii inayowazunguka..

Anasema, changamoto ya mabinti wanaioshi katika mazingira magumu, kwa kukosa elimu na waliamua kuandaa mafunzo ya kuwasaidia watoto walio katika mazingira magumu wajiendeleze katika ujasiriamali, utakaowainua kiuchumi.

Anasema, taasisi yao mpaka sasa imesaidia makundi mawili ya watoto wasio na elimu, kwa kuwawezesha stadi za kijasiriamali kuwainua kiuchumi.

Diwani Kipunguni

Diwani Kata ya Kipunguni, Mohamed Msofe, anasema kwamba kituo hicho ni mkombozi kwa watoto waishio katika mazingira magumu na kimekuwa chachu katika maendeleo ya kundi hilo.

Anasema, jamii inapaswa kuchangamkia fursa pale wanaposikia kuna nafasi bure kwa ajili ya kuwasaidia watoto walio na mazingira mabaya.

Msofe anaeleza kwamba, wanaokuwa na changamoto za kimaisha, inapotokea wakiwezeshwa wanaweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika maeneo yao wanayoishi.

Kwa mujibu wa diwani huyo, Kipunguni mpaka sasa ina wakazi zaidi ya 50,000 wanaojishughulisha na biashara kubwa na biashara ndogo, ikiwamo shughuli za mboga ambazo ni maarufu katika eneo hilo.

Mnufaika

Tatu Gasana, ni mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo anasema kuwa, yeye alimaliza Elimu ya Msingi mwaka Jana, lakini wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumwendeleza kielimu.

Anasema aliposikia tangazo la ujasiriamali hasa mafunzo kutolewa bure, alijisajili ili yamsaidie katika maisha yake.

Amina Ramadhan, mmoja wa mnufaika wa mafunzo hayo, anasema kuwa, mafunzo hayo yatamsaidia katika maisha yake pale atakapopata ujuzi.