Kardinali Pengo ang'atuka, Ruwa’ichi awa mrithi rasmi

16Aug 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kardinali Pengo ang'atuka, Ruwa’ichi awa mrithi rasmi

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Mtakatifu Francisko, ameridhia ombi la kustaafu, Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Wakati huo huo, Papa Francisko amemteua Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Ruwa’ichi, kuanzia sasa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo hilo.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk. Charles Kitima, ilieleza kuwa Balozi wa Baba Mtakatifu nchini, anataarifu kuwa kuanzia jana Baba Mtakatifu Fransis amekubali ombi la Kardinali Polycarp Pengo la kustaafu katika majukumu ya kuongoza Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

“Askofu Mkuu Ruwa’ichi ambaye mpaka sasa ni Askofu Mwandamizi, anachukua rasmi majukumu ya kuliongoza Jimbo Kuu la Dar es Salaam,” taarifa hiyo ilieleza.

Akizungumza na Nipashe, Padri Kitima alisema kwa utaratibu wanapostaafu, Kardinari Pengo hafungwi kwenda popote anakotaka, ingawa lazima akae kwenye jimbo.

“Kama ataamua kubaki Dar es Salaam hafungwi, akiamua kwenda jimbo alikobatizwa anaruhusiwa, popote atakapoamua yeye kwenda hakatazwi, ila hawezi kurudi nyumbani kwao bali atakaa kwenye jimbo lolote atakalolichagua ili akaishi huko,” alisema.

Alisema tangu kuanzishwa kwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam mwaka 1953, aliyeanza kuliongoza ni Askofu Mkuu, hayati Edgar Marantha na baada ya mwaka 1969 Hayati Laurian Kardinali Rugambwa.

 Kardinali Pengo alisimikwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo hilo Julai 22, mwaka 1992 baada ya kustaafu kwa mtangulizi wake, hayati Laurean Kardinali  Rugambwa.

ALICHOSEMA PENGO

KABLA YA KUSTAAFU

Agosti 5, mwaka huu, Kardinali Pengo akiwa katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 75 tangu kuzaliwa kwake, aliwaambia watu wa Mungu Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwamba, anasubiria wakati wowote kumtii Baba Mtakatifu Francisko atakapomwambia kupumzika katika utume wa kiaskofu.

“Nasubiria kumtii Mwenyezi Mungu wakati wowote atakaponiita na kuniambia pumzika kwa daima.

“Kuna kaburi langu pale Pugu, naomba liheshimiwe. Nawahisi viongozi wote wa kanisa, waumini na wengine wote, nikifa nizikwe kwenye kaburi langu la Pugu.

“Naamini katika karama ya utii, nikiwa Shemasi na umri wa miaka 26, Askofu Msakila (Sumbawanga) aliniambia nikipata upandre nitakuwa Katibu wa Jimbo, nilishtuka sana, baada ya miaka miwili nikaambiwa naenda Roma kufanya masomo ya juu, niliporudi nikafundisha Seminari Kuu ya Kipalapala mwaka 1977.” Kardinali Polycarp Pengo alisema siku hiyo.

Pia alisema baadhi ya wanafunzi wake ni Askofu Mkuu, Ruwa’ichi na Askofu Rweyongeza.

“Baadaye mwaka 1978 niliitwa TEC nikaambiwa natakiwa kuwa Gombera mwanzilishi wa Seminari Kuu ya Segerea, nilipokaa hadi mwaka 1984,” alieleza.

Aliongeza: “Sikuwahi kuwa kiongozi wa seminarini, ni mara moja kidogo pale seminari ndogo ya Kaengesa nilikuwa kiranja msaidizi. Lakini muda mwingi sikuwa kiongozi shuleni. Sasa sijui kwa nini Mungu alinipa kuongoza kanisa.

“Siyo mpenzi wa michezo hata kidogo, kiasi kwamba kule seminari ndogo nililazimika kucheza mpira kwa lazima ambao nilikuwa siuwezi pia, kwa sababu michezo ilikuwa lazima.”

Kardinali Polycarp Pengo alinukuliwa akisema: “Siamini kama nimewahi kufanya lolote, ni Mwenyezi Mungu amefanya kupitia kwangu na wenzangu wote.”

Kardinali Pengo alizaliwa Agosti 5, 1944 katika Parokia ya Mwazye, Jimbo Katoliki la Sumbawanga, aliingia seminari ya mwanzo ya Karema mwaka 1959 hadi 1964 na baadaye Seminari ya Kaengesa 1959 hadi 1964.

Alijifunza falsafa katika Seminari Kuu ya Kipalapala, Tabora mwaka 1965/67, Teolojia 1968/71 na elimu ya dini kutoka Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda.

Juni 20, mwaka 1971 alipewa daraja takatifu ya upadri na hayati Askofu Karolo Msakila katika Parokia ya Mwazye na kuteuliwa kuwa Katibu wa Jimbo hadi Julai mwaka 1973 alipotumwa Roma kwa masomo ya juu ya Teolojia ya Maadili.

Desemba mwaka 1977 hadi 1983 alitumwa na maaskofu kuwa Gombera mwanzilishi wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga, Segerea Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Novemba 11, mwaka 1983 aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Nachingwea na Januari 6, mwaka 1984 kuwekwa wakfu na Baba Mtakatifu mwenyewe (Mtakatifu Yohane Paulo IIII) Roma na kusimikwa Februari 19, mwaka 1984.

Habari Kubwa