Mkapa atoa angalizo vijana kukosa ajira 

16Aug 2019
Gwamaka Alipipi
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mkapa atoa angalizo vijana kukosa ajira 

RAIS mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, amewataka viongozi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuwekeza zaidi katika kuwajengea uwezo vijana ili wajiajiri.

RAIS mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa

Amesema viongozi wa SADC wanapaswa kuwajengea mazingira mazuri ya kupata ajira vijana ambao ndiyo idadi kubwa ili waziendeleze rasilimali zilizoko katika nchi zao.

Mkapa alitoa rai hiyo jana katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wakati akiongoza mjadala wa kikanda wa mtangamano wa SADC.

"Idadi kubwa ya wananchi wa SADC ni vijana, tunapaswa kuwaandaa vyema, elimu yetu inapaswa kuwaandaa katika kujiendeleza wenyewe, wanapaswa kujengwa katika ujuzi na uchumi wa kidijitali," Mkapa alishauri.

"Ili kufanikisha hayo, ni lazima kuwapo kwa ushirikiano wa pamoja baina ya sekta binafsi na serikali katika kusaidia utekelezaji wa sera ya kutokomeza umaskini miongoni mwa nchi wanachama pamoja na mabadiliko ya teknolojia."

Mkapa pia alisema kuna haja kutolewa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa SADC na kuendeleza mikakati kama vile kuchochea ushirikiano baina ya viongozi, akieleza kuwa ndiyo njia pekee ya kufikia uchumi huru.

Alisema miongoni mwa mambo ambayo SADC imefanikiwa kwa kiasi kikubwa ni kuimarisha amani na usalama miongoni mwa nchi wanachama.

"Hata hivyo, bado kuna changamoto ambazo nimeziona zinaikabili jumuiya hii kama vile umaskini miongoni mwa jumuiya, uzalishaji mdogo wa bidhaa na ubovu wa miundombinu," Mkapa alisema.

Alisema umoja na mshikamano kati ya viongozi wa jumuiya hiyo ndiyo utasiaidia kuondoa vikwazo hivyo, akibainisha kuwa changamoto zilizopo sasa ni tofauti na za miaka iliyopita.

Mkapa pia aliwataka viongozi wa SADC kutafuta wawekezaji wazuri watakaowekeza kwenye viwanda na teknolojia.

Katika mjadala huo, Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. Willium Anangisye, alisema: "Sisi, UDSM tunafurahi kusikia kuwa mojawapo ya lugha ya mawasiliano itakayotumika katika vikao vya SADC ni Kiswahili, hata sisi hapa chuoni tumeanza jitihada za kukitangaza Kiswahili kwani tuna idara inayofundisha lugha hiyo."