Hasunga: Tutaimarisha biashara ya mazao SADC

16Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hasunga: Tutaimarisha biashara ya mazao SADC

SERIKARI imesema kuwa imejipanga kuimarisha biashara ya mazao ya kilimo na mengineyo kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ili kuwanufaisha wakulima katika nchi hizo.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi 16 wanachama wa SADC. Alisema kuwa zaidi ya Watanzania milioni 50 wanategemea chakula, hivyo lazima kubadili mbinu za uzalishaji katika mazao ya kilimo kwa kuongeza tija kupitia teknolojia mpya ili kuwa na uzalishaji mkubwa na wenye tija. Waziri Hasunga alisema kuwa malighafi zinazohitajika zaidi ya asilimia 66 zinatokana na mazao ya kilimo, hivyo ukamilisho wa serikali ya viwanda unaungwanishwa kwa ukaribu na sekta ya kilimo. Kwa mujibu wa Hasunga, Mkutano wa SADC ni fursa kwa wakulima wa Tanzania kwa kuwa wageni wote waliowasili na watakaoendelea kuwasili watahitaji kula vizuri, hivyo mkutano huo ni sehemu ya kuimarisha na kutangaza masoko ya mazao mbalimbali hususani vyakula vya asili. Aidha, utoshelevu wa chakula nchini ni asilimia 119 ukilinganisha na mwaka jana ambapo ulikuwa asilimia 124, hivyo serikali imefungua mipaka ya kuuza mazao nje ya nchi, lakini pia ni lazima kuwa na kumbukumbu muhimu za taarifa zote za usafirishaji wa mazao. Waziri Hasunga alisema ni wakati mwafaka kwa nchi za Afrika Mashariki na nchi zote za SADC kuanza kutumia masoko ya ndani ya nchi katika mazao ya kilimo na mengineyo kuliko kutegemea kuagiza katika nchi zingine nje ya Afrika. 

Alisema kuwa kufanya hivyo kutaimarisha masoko ya mazao mbalimbali nchini, hivyo kuwaimarisha wakulima katika kilimo chao, na kuwa na kipato kikubwa kinachokidhi mahitaji ya kila mkulima pamoja na uimara wa uchumi wa nchi.

Habari Kubwa