Wawekezaji wa Afrika Kusini wakaribishwa

16Aug 2019
Beatrice Moses
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wawekezaji wa Afrika Kusini wakaribishwa

RAIS John Magufuli amewakaribisha wawekezaji kutoka Afrika Kusini kuwekeza viwanda vya nguo, viwanda vya dawa na vya magari, na maeneo mengine yatakayowavutia.

RAIS John Magufuli

Akizungumza jana wakati wa mkutano wa Baraza la Wafanyabiashara wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini, alisema mahitaji ya kutengeneza nguo kwa pamba inayozalishwa  nchini, pamoja na mazao ya nyama, wanaweza pia kuzalisha viatu na bidhaa zingine zitokanazo na ngozi.

Alisema lengo ni kupunguza bidhaa ghafi zinazokwenda nje ambazo zikitumika katika nchi husika, zitaweza kuzalisha ajira nyingi kwa vijana.

“Milango ipo wazi kwa ajili ya wawekezaji, tuna samaki katika bahari na maziwa, tunataka kufikia mahali ambapo tunaweza kuzalisha bidhaa zetu hapahapa ndani ya nchini,” Rais Magufuli alisema.

Alielezea jinsi serikali yake ilivyojipanga katika kukuza sekta ya viwanda na uwekezaji, imeandaliwa mifumo wezeshi kuwezesha Tanzania kufanikiwa kuwa ya viwanda.

Alitaja baadhi ya miradi ambayo imewekwa kwenye mfumo wezeshi wa viwanda  ni  kuboresha upatikanaji wa nishati katika bonde la Rufiji, ujenzi wa miundombinu ukiwamo ujenzi wa viwanja vikubwa vya ndege, barabara na reli

Rais Magufuli alieleza jinsi serikali anayoiongoza ilivyoweza kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na kuwezesha kununuliwa kwa ndege kadhaa, hivyo kuwa na usafiri wa anga unaoanzia nchini.

“Zipo ndege zinazokwenda  Afrika Kusini mara nne kwa wiki, hii itasaidia kuwezesha biashara na uwekezaji, lakini pia kukuza utalii wa ndani kati ya nchi zetu mbili, bandari nazo zinatanuliwa na kujengwa,” alisema.