TADB yaasa taasisi za fedha SADC

16Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
TADB yaasa taasisi za fedha SADC

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), imesema fedha ya uhakika ya kujenga miundombinu ya maendeleo katika nchi za SADC itatoka ndani na hasa itapatikana kwa kujenga ubia wa kimkakati baina ya taasisi za fedha zilizomo katika jumuiya hiyo.

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB),

Pia imeshauri kukazania kuongeza thamani mazao ya kilimo.

Akiwasilisha mada jijini Dar es Salaam katika mkutano wa nne wa mwaka wa maendeleo ya viwanda katika nchi za Jumuiya ya

Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),  Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine, alisema historia inathibitisha kwamba nchi za Afrika hazitofanikiwa katika shabaha yake ya kujenga miundombinu ya maendeleo iwapo zitategemea fedha kutoka nje ya bara hili.

“Tutaongeza minyororo ya thamani ya mazao ya kilimo katika nchi za jumuiya yetu iwapo tutaenzi kila aina ya ubia wa kimkakati baina yetu. Sisi TADB milango yetu iko wazi. Tuko tayari kuzungumza na taasisi ya fedha ya aina yoyote katika kanda yetu juu ya njia bora kujenga ubia wa kimkakati na wenye tija,” Justine amezihakikishia nchi wanachama wa SADC.

Aliwaambia wajumbe hao kwamba umuhimu wa kuwapo kwa fedha ya kujenga miundombinu ya maendeleo katika Afrika unajulikana, lakini aliongeza kwamba kwa bahati mbaya kuna pengo kubwa kati ya mahitaji na fedha iliyopo ili kujenga miundombinu hiyo.

Alisema makadirio ya pengo ni dola za Marekani bilioni 130 kwa mwaka, lakini yawezekana makadirio

halisi ni dola 170 bilioni kwa mwaka.

Justine alisema uwezo uliopo kuzipa pengo hilo ni kidogo, sana

sana ni uwezo wa kuziba nusu ya pengo hilo au usifikiwe.

Misaada rasmi (ODA) nayo imekuwa ikiporomoka toka 2013 na mitaji ya uwekezaji (FDI) kuingia Afrika nayo imekuwa ikiporomoka toka mwaka huo, alieleza.

Alishauri zifanywe jitihada za kutafuta vyanzo mbadala na mifano ya kugeuzwa katika kupata fedha ya kujenga miundombinu ya maendeleo na viwanda.

Kwa mujibu wa Justine, fursa zilizopo kwa sasa ni kujitahidi kupata fedha kutoka mifuko ya jamii, mifuko inayojitegemea, kampuni za bima na hata watu binafsi wenye uwezo.

Amewakumbusha wajumbe umuhimu wa kilimo katika kuiendeleza Afrika, na SADC na kusema  kwa bahati mbaya kilimo kimekuwa kikipewa fedha kidogo sana na wakulima wadogo wamekuwa hawapewi msukumo wa kutosha kuzalisha mazao kwa tija.

“Afrika ina uwezo wa kuilisha dunia kwani nusu ya ardhi murua kwa kilimo ya dunia na ambayo haitumiki iko Afrika. Afrika ina maji mengi. Lakini Afrika inatumia dola bilioni 35 za Marekani kununua chakula kutoka nje kila mwaka. Afrika inaweza kuilisha dunia ikiwa itawajali wakulima wadogo ili kilimo kiwe na tija na endelevu,” alisema.

Habari Kubwa