Ndugai aomba muda kumjibu Lissu

16Aug 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ndugai aomba muda kumjibu Lissu

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imesema Ijumaa ya wiki ijayo itasikiliza ombi la muda la kuzuia kuapishwa kwa Mbunge Mteule wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu (CCM), itakaposikiliza maombi ya kupinga kuvuliwa ubunge wa jimbo hilo, yaliyofunguliwa na Tundu Lissu aliyekuwa mbunge wake.

Vilevile, upande wa walalamikiwa katika kesi hiyo umeomba mahakama iwape muda wa kuandaa majibu ya kiapo kinzani ili kupata busara za Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mahakama hiyo imepanga kusikiliza maombi ya msingi ya Lissu dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Agosti 23, mwaka huu, mbele ya Jaji Sirilius Matupa.

 

Jaji huyo alisema ombi hilo la kuzuia kuapishwa kwa mbunge mteule limo ndani ya maombi ya msingi na lina hoja nyingi za kikatiba na kisheria na kwamba mahakama yake haina taarifa kuhusu Bunge kuanza vikao ndani ya siku 14 zijazo vitakavyowezesha mbunge huyo kuapishwa.

Alisema mahakama yake itasikiliza maombi yote na uamuzi utatolewa.Upande wa mlalamikaji uliongozwa na mawakili; Peter Kibatala, Jeremiah Mtobesya na Omary Msemo.

Awali, Kibatala aliomba mwongozo wa mahakama hiyo kama itaweza kusikiliza ombi hilo na kutoa amri ya muda ya kuzuia uapishwaji wa Mtaturu.

Alidai lengo la ombi hilo ni kulinda maana ya maombi ya msingi ambayo wajibu maombi wataenda kuyajibu.

Hata hivyo, upande wa walalamikiwa ulioongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Vicent Tangoh, uliomba ombi dogo na ombi la msingi yasikilizwe kwa pamoja.

Upande huo wa walalamikiwa pia uliomba mahakama iwape muda wa kuandaa majibu ya kiapo kinzani ili upate busara za Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

"Mtukufu Jaji, maombi haya yanagusa mhimili mwingine wa serikali, hivyo tunaomba muda tupate ushauri wao ili tuandae majibu ya kiapo hicho kinzani," Tangoh alidai.

Wakili huyo wa walalamikiwa alidai atawasilisha majibu ya kiapo kinzani Agosti 21 na wakili wa mlalamikaji atawasilisha hoja za nyongeza Agosti 22 na mahakama itasikiliza maombi hayo Agosti 23, mwaka huu.

Kwa mujibu wa maombi hayo namba 18 ya mwaka huu, Lissu anaiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili mahakama hiyo itoe amri ya kumtaka Spika Ndugai ampe (Lissu) taarifa yake ya kumvua ubunge.

Pia, mtaalamu huyo wa sheria anaiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili mahakama hiyo iite taarifa ya uamuzi wa Spika wa kumvua ubunge na kisha itengue na kutupilia mbali uamuzi huo wa Spika Ndugai kumvua ubunge.

Mwombaji huyo pia anaomba mahakama impe kibali afungue shauri ili mahakama itoe amri ya kusimamisha kuapishwa kwa Mbunge Mteule wa Jimbo la Singida Mashariki, Mtaturu.

Katika hati ya dharura, Lissu anaiomba mahakama hiyo isikilize na kutoa uamuzi wa maombi yake haraka vinginevyo, Mtaturu ambaye Julai 19, mwaka huu alitangazwa mshindi na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, ataapishwa kushika wadhifa huo.

Lissu anadai atakuwa ameathirika kwa kuwa atapoteza haki zake zote, kinga na maslahi yake yote yanayoambatana na wadhifa wake huo wa ubunge.

Uamuzi wa kumvua ubunge Lissu ulitangazwa na Spika Ndugai Juni 28, mwaka huu, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, akitaja sababu mbili.

Spika Ndugai alizitaja sababu hizo kuwa ni kushindwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na sababu ya pili ikiwa ni kutokujaza taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.