RAS atengua uamuzi wa DC watumishi kulipia ultra sound

16Aug 2019
Happy Severine
BARIADI
Nipashe
RAS atengua uamuzi wa DC watumishi kulipia ultra sound

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini, ametengua uamuzi uliotolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga wa kuwataka watumishi 137 wa Hospitali ya Halmashauri ya mji wa Bariadi (Somanda) kuchanga fedha na kulipia mashine ya ultra sound iliyoibwa.

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini

Sagini alitengua uamuzi huo wakati akiongea na watumishi wa hospitali hiyo na kueleza kuwa jambo hilo haliwezi kuwa la kila mtumishi kwa kuwa sio wote walioshiriki katika tukio hilo.

Alisema ni vema na lazima wakatafutwa wahusika na wizi huo ili waweze kurejesha mashine hiyo na si kuwaadhibu watumishi wote.

Sagini alisema, mkoa umeangalia na kubaini kuwa sio watumishi wote 137 wa hospitali hiyo walioshiriki katika wizi huo kwa kuwa wengine walikuwa mapumziko, likizo hivyo si haki kuhukumu wote.

“Awali DC wangu aliwauliza watumishi kama wanatambua mhusika wa wizi sambamba na kuwapigisha kura za siri, lakini hakuna aliyekubali kubaini wapi ilipo ultrasound au kumtambua mhusika na ndipo DC akaamua kuchukua hatua ambazo ni sahihi, lakini kama mkoa tunasikitishwa na kitendo hiki cha wizi wa mashine hiyo, ukizingatia tumewakabidhi hospitali hata mwezi haujaisha kimeibiwa...pia tutambue kuwa sisi tuna vyombo vya dola ambavyo vina watu wanalipwa kwa shughuli hii, hivyo nawaomba wahusika warejeshe kifaa hicho,” alisema Sagini.

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali, Catherine Dickson, alisema uamuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi wa kuwataka watumishi wote kulipa kifaa hicho kimsingi ni kinyume na utaratibu  kisheria na kwamba wanaushukuru uongozi wa mkoa kwa kutambua sheria, kanuni na taratibu kwa  kusitisha uamuzi huo na kuviachia vyombo vya sheria vifanye kazi yake.

Naye mmoja wa watumishi wa hospitali hiyo, Flora  Katoyo, ambaye anahudumu kitengo cha dawa, alisema ameshukuru tamko hilo lililotolewa na uongozi wa mkoa kwa kuwa limekuwa  faraja kwao.

"Jana nimelala vibaya pressure (shinikizo) ipo juu mpaka sasa kichwa kinaniuma...uwezo wangu ni mdogo, kwanza kifaa chenyewe sikijui tunaambiwa wote tulipe yaani naongea kwa uchungu mpaka nasikia kulia kwa furaha niliyonayo baada ya tamko hili la katibu tawala," alisema Katoyo.

"Tulipopata taarifa jana utendaji kazi ulipungua kwa sababu mtu anafanya kazi huku akijua kuna makato leo morali ya kazi imerudi, awali tulikuwa na mawazo sana,” alisema Simon Chisomeko.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi alitoa siku saba kwa watumishi wa hospitali hiyo kuchanga na kuhakikisha mashine hiyo yenye thamani ya Sh. milioni 30 inapatikana.

Habari Kubwa