Majeruhi wengine 7 ajali ya lori la mafuta wafariki

16Aug 2019
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Majeruhi wengine 7 ajali ya lori la mafuta wafariki

MAJERUHI wengine saba katika ya 46 waliopokelewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kujeruhiwa katika ajali ya lori la mafuta eneo la Msamvu mkoani Morogoro, wamefariki dunia, hivyo kuifanya idadi ya waliopoteza maisha kutokana na ajali hiyo kufika 89.

Pia idadi ya majeruhi wa ajali hiyo, waliofariki dunia wakipata matibabu MNH sasa imefika 21. Majeruhi hao walifikishwa kwenye hospitali hiyo Jumamosi.

Imeelezwa kuwa majeruhi wengine 16 kati ya 25 wanaoendelea kupata matibabu katika hospitali hiyo kubwa zaidi nchini, hali zao ni mbaya.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa MNH, Aminiel Aligaesha, alisema wagonjwa hao 16 wako katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).

"Kati ya majeruhi 46 waliofikishwa Muhimbili, tunasikitika kuwaeleza kuwa waliofariki dunia hadi leo (jana) alfajiri wamefika 21, waliobaki sasa ni 25, tunaomba tuendelee kuwaombea madaktari ambao wanaendelea kuwapatia matibabu wagonjwa waliobaki," Aligaesha alisema.

Aliongeza kuwa wagonjwa waliosalia wanaendelea kupatiwa matibabu ili kuokoa maisha yao.

Aligaesha aliwataja waliopoteza maisha juzi kuwa ni Ramadhani Mdoe (50), mkazi wa Mwembesongo, Shabani Maringanya (40), mkazi wa Ifakara, Shabani Ayoub (34), mkazi wa Morogoro, Khalifa Iddy (26), mkazi wa Msamvu, Omary Omary (26), mkazi wa Morogoro, Omary Abdallah (24), mkazi wa Msamvu na Aloyce Mponzi (36), mkazi wa Kihonda.

Alisema miili yote imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo kwa ajili ya maandalizi ya kusafirishwa kwenda mkoani Morogoro kwa maziko.

"Miili yote ipo chumba chetu cha kuhifadhi maiti na leo jioni (jana) itasafirishwa kuelekea mkoani Morogoro kwa ajili ya maziko," Aligaesha alisema.

Ofisa huyo wa MNH alisema miili ya watu sita waliopoteza maisha juzi, ilisafirishwa jana kuelekea Morogoro kwa ajili ya maziko yatakayofanyika kwenye eneo maalum lililotengwa na serikali.

Aligaesha alisema serikali imeandaa utaratibu wa kuisafirisha miili hiyo hadi mkoani Morogoro katika eneo hilo maalum la maziko lililoandaliwa.

Alisema serikali pia inagharamia jeneza na sanda kwa ajili ya miili yote ya watu waliopoteza maisha kutokana na tukio hilo.

"Kwa ndugu ambao wanataka kuchukua miili ya wapendwa wao kwenda kuzika mikoa mingine mbali na eneo ambalo serikali imetenga mkoani Morogoro, watajigharamia usafiri na wataendesha taratibu nyingine wenyewe," Aligaesha alisema.

CHUPA 400 ZA DAMU

Aligaesha pia alisema idadi ya wananchi waliojitokeza kwa ajili ya kuchangia damu inazidi kuongezeka na kwa siku nne hadi juzi, walikuwa wamekunywa takribani chupa 400.

Aliwataka watu wenye mapenzi mema kuendelea kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya majeruhi wengi ambao wanahitaji damu kwa wingi.

Ofisa Mhamasishaji Damu wa MNH, John Bigambalaye, alisema kwa siku kiwango cha damu kinachohitajika kwa wagonjwa wao na Mloganzila ni chupa 150.

Alisema MNH pekee wanatumia chupa 120 kwa siku za kawaida na inapotokea majanga kama ya ajali ya moto, wanatumia chupa hadi 200 za damu kwa siku.

Alisema kwa siku hizo nne ambazo makundi ya watu mbalimbali yanajitokeza kuchangia damu, wamekusanya hadi chupa 120 tofauti na awali walipokuwa wakikusanya chupa 80 kwa siku.

Bigambalaye alisema majeruhi hao wa moto wanahitaji zaidi maji yanayotoka kwenye damu na chembechembe za damu.

Imeandikwa na Mary Geofrey na Mariam Magili