Mbivu mbichi ushahidi wa video kesi Mbowe, wenzake Jumatatu

16Aug 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mbivu mbichi ushahidi wa video kesi Mbowe, wenzake Jumatatu

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imepanga kutoa uamuzi wa kukubali au kukataa ombi la Jamhuri la kuonyesha tukio kwa njia ya runinga Agosti 19, mwaka huu, katika kesi ya uchochezi-

Freeman Mbowe.

-inayowakabili vigogo tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwamo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe.

Uamuzi huo ulipangwa kutolewa jana lakini mawakili wa utetezi walikuwa na kesi nyingine Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Hata hivyo, Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, alisema mahakama yake itatoa uamuzi na itaendelea kusikilizwa Agosti 19.

Awali, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Faraja Nchimbi, Dk. Zainabu Mango na Wakili wa Serikali Jacqueline Nyantori, ulidai kuwa uko tayari kuendelea lakini mawakili wa utetezi wana kesi nyingine Mahakama Kuu.

Hakimu alisema washtakiwa wote wataendelea kuwa nje kwa dhamana na kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Jumatatu ijayo.

Mapema mahakamani hapo, shahidi wa sita Koplo Charles wa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, alidai kuwa alikimbilia kwenye gari la jeshi hilo kunusuru kamera yake ya video.

Aidha, alidai mihemko hiyo ilisababishwa na hamasa aliyoitoa Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe, kutoa kauli ya kuwapandikiza chuki wafuasi hao dhidi ya serikali.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi, shahidi alidai kuwa Februari 16, mwaka jana, alipangiwa kazi kama mwandishi wa habari katika mkutano wa kufunga kampeni wa Chadema katika viwanja vya Buibui, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Alidai kuwa alijiandaa na vitendea kazi vyake ikiwamo kamera ya kupiga picha za video na ilipofika saa 10:00 alasiri, alikuwa katika viwanja hivyo kwa ajili ya kuanza kazi.

"Nilipofika watu walianza kukusanyika na mshereheshaji alitangaza kwamba viongozi wakuu wa chama wameshafika. Baada ya muda wabunge na viongozi wakuu walipanda jukwaani, nilimsikia Mbowe akitoa kauli za kufanya hamasa ya kuichukia serikali," alidai na kuongeza kuwa:

"Wanachama walipata hamasa na mihemko iliyosababisha wapate jazba ya kuichukia serikali na vyombo vya ulinzi na usalama. Wananchi waliokuwa wamekaa walinyanyuka na kuhamasika, mimi na waandishi wenzangu tulitawanyika pale tuposimama karibu na jukwaa, nilikimbilia kwenye gari la polisi kunusuru kamera," alidai Koplo Charles.

Jopo la utetezi liliongozwa na Wakili Profesa Abdallah Safari, Peter Kibatala, John Mallya na Hekima Mwasipu.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Bunda Mjini, Ester Bulaya; Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji; Mbunge wa Iringa Mjini; Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka jana, Mbowe na wenzake wakiwa Kinondoni, kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawakuwapo mahakamani, kutenda kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka jana, Bulaya alishawishi kutenda kosa la jinai katika viwanja vya Buibui kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Ilidaiwa Februari 16, katika barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni, Kinondoni, kwa pamoja washtakiwa na wenzao zaidi ya 12 walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa Jeshi la Polisi, Gerald Ngiichi, na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili, Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.

Ilidaiwa siku ya tukio la kwanza na la pili, katika viwanja vya Buibui kwenye mkutano wa hadhara, Heche alitoa lugha ya kuchochea chuki alitamka kwamba: "Kesho patachimbika, upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii, wizi unaofanywa na serikali ya awamu ya tano, watu wanapotea, watu wanauawa wanaokotwa kwenye mitaro lazima ukome.”

Washtakiwa wote waliposomewa mashtaka yao kwa nyakati tofauti walikana.