Malinzi ajitetea, anaidai TFF deni la mil. 152.6/-

16Aug 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Malinzi ajitetea, anaidai TFF deni la mil. 152.6/-

RAIS wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, amedai mahakamani kwamba wakati wa uongozi wake mpaka alivyokamatwa na kushtakiwa bado analidai shirikisho hilo zaidi ya Sh.  milioni 152.6.

RAIS wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi

Malinzi anayekabiliwa na mashtaka ya kughushi na kutakatisha fedha aliwasilisha jana taarifa ya benki ya mwaka 2014 na risiti 13 zilizoonyesha TFF kumlipa Malinzi fedha za mkopo alizokuwa anawadai.

Ushahidi wa utetezi wa kigogo huyo ulisikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Maira Kasonde.

Mbali na Malinzi washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga na Karani Flora Rauya.

Akiongozwa na Wakili Richard Rweyongeza, Malinzi alidai katika taarifa ya benki ya kuanzia Januari, 2014 hadi Agosti 19, 2014 alikuwa anaidai Sh. 152,613,004.83 na kwamba kuna Dola za Marekani 5,000 ambazo alizitoa nchini Msumbiji hazikuingizwa kwenye mfumo huo badala yake waliingiza kwa mkono.

Alidai fedha hizo zilipobadilishwa kuwa Shilingi, jumla ilikuwa Sh. milioni 8.3 na kwenye taarifa hiyo waliandika kuwa “kiasi unachotudai kwa mujibu wa kumbukumbu zetu ni Sh. 152,613,004.83.”

Malinzi alidai uingizaji wa fedha hizo ulikuwa kwa njia mbalimbali ni kuweka kwenye akaunti za TFF na kutoa fedha taslimu kwa Shilingi au Dola.

Alidai alipokuwa anapewa fedha walikuwa wakimpa risiti kwa majina yake na kwamba aliendelea kutoa fedha hadi alipokamatwa mwaka 2017.

“Kati ya risiti hizo, nilizo nazo zilisainiwa na Hellen Adam ambaye alikuwa shahidi wa 10 wa upande wa mashtaka na Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Daniel Msangi, ambaye alikuwa shahidi wa sita. Risiti nyingine haikuwa na saini, lakini kwenye taarifa ya benki ilionyesha imeingizwa kama mkopo,” alidai.

Pia alidai kuwa risiti zote zinatunzwa na idara ya uhasibu ya TFF na kwamba amekuwa akilipwa kwa mafungu mafungu kutokana na hali ya shirikisho hilo kuwa mbaya kiuchumi.

Aliendelea kudai kuwa idara ya fedha ilikuwa ikikaa na kuangalia namna ya kumlipa kutokana na kile wanachokipata.

“Mheshimiwa hakimu nilikuwa nalipwamadeni yangu pale tu TFF ilipopata fedha za ruzuku kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) au Shirikisho la Mpira Afrika (CAF) au kutoka kwa wafadhili kama ilivyokuwa kwa Kampuni ya Bia ya Serengeti na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL),” alidai Malinzi.

Malinzi alidai mwaka 2015 hali ya TFF ilikuwa haijabadilika kwa hiyo  alikuwa akitoa fedha zake mfukoni na kuwaomba wadau mbalimbali kuendelea kuchangia na mwishoni mwa mwaka 2014 alijenga ofisi ya rais na nyaraka alizokuwa anatunza nyumbani alianza kuzitunza ofisini.

Alidai Julai, 27 alikamatwa na alilala polisi kwa siku mbili mfululizo na Julai 29, alifikishwa mahakamani, hivyo hakuwahi kuingia tena ofisi za TFF.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Kasonde aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 27, mwaka huu, kwa ajili ya utetezi.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 213 ya mwaka 2017, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 20 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa Dola za Marekani 173,335.