Mabalozi waona fursa uwanja wa ndege Dar

17Aug 2019
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mabalozi waona fursa uwanja wa ndege Dar

MABALOZI wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa 42 duniani, wamesema kukamilika kwa ujenzi wa jengo la tatu la abiria la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kutafungua fursa za uchumi nchini.

Wamesema watalii wengi pia watakuja nchini kwa sababu ndege kubwa zitatua, wawekezaji wa viwanda watajitokeza kutokana na kuwapo kwa umeme wa uhakika kupitia mradi wa kufua umeme wa maporomoko ya maji katika Mto Rufiji na miundombinu ya usafiri kama mradi wa reli ya kisasa (SGR).

Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam walipotembelea jengo la tatu la uwanja huo, mabalozi hao walisema utatangaza taswira ya Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani hasa wakati huu ambao marais wa nchi 16 watakuwa nchini kushiriki Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Balozi wa Tanzania Ujerumani, Dk. Abdallah Possi, alisema amepata bahati ya kutembelea viwanja vingi duniani na kwa jinsi JNIA ulivyotengenezwa anaamini kutafungua fursa mbalimbali za uwekezaji.

Alisema kazi ya mabalozi ni kutangaza vivutio vilivyopo nchini ili kuwavutia wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali.

Balozi wa Tanzania Sweden, Dk. Willibrod Slaa, alisema kuanza kutumika kwa jengo hilo la tatu la JNIA kutasaidia kuwa na mvuto na kuleta wawekezaji na watalii wengi zaidi na hivyo kukuza uchumi wa taifa.

Alisema ili kufikia malengo tarajiwa, Tanzania inapaswa kujifunza kwa mataifa mengine yaliyofanikiwa kwa sababu haiwezi kufanikisha kila kitu kwa wakati mmoja.

Balozi wa Tanzania Malaysia, Ramadhani Dau, alisema uwanja huo una vigezo vya kimataifa hivyo ni fursa nzuri kwao kuendelea kuitangaza Tanzania duniani kote.

Balozi wa Tanzania India, Baraka Luvanda, alisema fursa nyingi zimeendelea kufungua milango ya uwekezaji nchini hasa kuanza kwa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Mumbai.

"Kuwapo kwa safari hii kumefungua milango ya kukuza uchumi, imerahisisha usafiri kwa raia wa India na Tanzania ambao watazidisha ushirikiano katika sekta mbalimbali," Balozi Luvanda alisema.

Balozi wa Tanzania Cuba, Valentino Mlowola, alisema kuwapo kwa uwanja huo ni hatua kubwa na serikali inahitaji pongezi kwa kufungua milango ya kukuza uchumi.

Alisema Cuba wanatembelewa na watalii milioni tano kwa mwaka, hivyo kuwapo kwa uwanja huo ni kigezo cha kuwashawishi kuja nchini kutembelea vivutio vilivyopo.

Alisema pia watashirikiana na Cuba kujifunza mbinu mbalimbali zitakazowezesha watalii kutembelea vivutio mbalimbali nchini.

Awali, akielezea mradi huo, Mkurugenzi wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Patrick Mfugale, alisema jengo hilo lina uwezo wa kuhudumia watu 2,800 kwa saa moja na watu milioni nane kwa mwaka.

Alisema eneo la maegesho ya ndege linaweza kuegesha ndege 19 za daraja C na 11 daraja E na gharama za mradi huo ni Sh. bilioni 707 na tayari Mkandarasi ameshalipwa Sh. bilioni 680.

Imeandikwa na Mary Geofrey na Gidion Msabula

Habari Kubwa