Watoto wapigania uhuru walilia mafao

17Aug 2019
Christina Haule
Morogoro
Nipashe
Watoto wapigania uhuru walilia mafao

UJIO wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, nchini Tanzania umeibua mijadala kwa jamaa za waliokuwa wakimbizi katika makazi ya Mzimbu, Kampasi ya Solomon Mahlangu, wakidai kupewa mafao kutokana na vifo vya wazazi wao.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa

Jamaa hao walisema hayo jana wakati wakizungumza kwenye ujio wa Rais Ramaphosa kwenye kambi ya Solomon Mahlangu Mazimbu mkoani hapa. Miongoni mwa jamaa hao ni watoto walioachwa na wazazi wao (baba) walioondoka baada ya kurejea kwao mwaka 1992 na kubaki nchini huku wazazi wao wa kike pekee wakiendelea kuwahudumia.

Mmoja wa watoto walioachwa na baba yake, Omuto Elias Omathe (21), alisema  hajawahi kumwona baba yake licha ya kwamba mama yake alishawahi kumwambia kuwa ameshafariki dunia  akiwa Afrika Kusini.

Binti huyo ambaye hakuvumilia na kuamua kumwita Rais Ramaphosa alipokuwa akiondoka kutoka kwenye eneo la makaburi ya wapigania uhuru hao na kuangua kilio akimwomba Rais huyo kuwasaidia watoto kama yeye kupata fursa mbalimbali sambamba na wengine kuwajua wazazi wao kwakuwa waliondoka wakiwa wadogo.

Alisema wako wengi wanaoishi Tanzania na wamekosa fursa mbalimbali ambazo wenzao wanazipata zikiwamo elimu na makazi bora na kuwafanya kujiona kama hawana ndugu.

Omathe aliiomba serikali ya Afrika Kusini kuwawezesha kupata mafao kutokana na baba yake alikuwa mpigania uhuru ambaye aliondoka na kurejea nchini humo na kumwacha akiwa mdogo.

Alisema wakipewa mafao kama vile wanavyopewa wengine ambao baba zao wamefariki dunia wakiwa wapigania uhuru nchini humo na serikali inaendelea kuwahudumia, itawasaidia kujikimu katika mahitaji mbalimbali.

Naye mama wa binti huyo, Monica Omathe, alisema amefanya kazi za ndani katika kampasi hiyo muda mrefu tangu mwaka 1981 na kwamba alikutana na baba huyo na kukaa naye lakini baada ya mzazi mwenzie kuondoka, walihamishwa kwenye kambi walizokuwa wanakaa.