Ma-DED kikaangoni vitambulisho wajasiriamali

17Aug 2019
Said Hamdani
LINDI
Nipashe
Ma-DED kikaangoni vitambulisho wajasiriamali

MKUU wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, amewataka wakurugenzi wa halmashauri za manispaa na wilaya mkoani mwake kukamilisha uuzaji wa vitambulisho vya wajasiriamali ndani ya mwezi mmoja kuanzia juzi.

MKUU wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi

Kiongozi huyo wa mkoa alitoa agizo hilo juzi katika kikao kazi cha watumishi wa halmashauri kilichofanyika kwenye Uwanja wa Ilulu mjini Lindi.

Zambi alisema amelazimika kutoa muda huo kutokana na kusuasua kwa uuzwaji wa vitambulisho hivyo. Mkoa wa Lindi ulipatiwa vitambulisho 65,000.

Alisema hajaridhishwa na mwenendo wa uuzwaji wa vitambulisho hivyo ikizingatiwa uuzaji wake ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli.

Alisema mtendaji yeyote kuanzia ngazi ya mtaa, kijiji, kata, tarafa hadi wilaya atakayeshindwa kukamilisha uuzwaji wa vitambulisho hivyo kwa muda wa mwezi mmoja alioutoa, ni vema akajiondoa na kupisha walio na uwezo wa kufanya kazi hiyo.

Alisema ameshangazwa kuona mtumishi anapewa vitambulisho 300 lakini anauza 52, jambo alilodai ni uzembe.


Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, akizungumza katika kikao hicho, alimhakikishia Zambia kuwa vitambulisho vilivyobaki wilayani mwake vitakuwa vimeshauzwa kufikia mwishoni mwa mwezi huu.

Vitambulisho hivyo vilivyotengenezwa na Ofisi ya Rais vinauzwa kwa wajasirimali wadogo (mapato ghafi ya chini ya Sh. milioni nne kwa mwaka) kwa bei ya Sh. 20,000 kwa kila kitambulisho.

Habari Kubwa